
Pesa alizozipata hakuziwekeza kwa namna yoyoye ile na jina lake kubwa katika soka likamfanya awe na marafiki wengi huku wanawake wengi walionusa harufu ya pesa wakigombania kuwa karibu yake.
Hatimaye kipaji chake cha kusakata gozi la ng’ombe kilipopotea miguuni mwake kutokana na unywaji wa pombe uliopitiliza na kuwaendekeza wanawake.
Fashanu alikuwa akikesha baa na kuwa na wanawake wengi kiasi cha kumfanya kushindwa kucheza mpira katika kiwango chake. Alipoachwa na klabu zilizokuwa zikimtegemea hata marafiki aliokuwa nao karibu walimkimbia na mabibi hawakuta tena kuwa naye karibu kama zamani.
Kila alipopita mitaani watu walimbeza na kumwonyesha vidole kutokana na kufilisika kiasi cha kushindwa hata kulipa kodi ya nyumba.
Fashanu aliishia kudhalilika kwa kulala katika vibarazani vya nyumba za watu waliokuwa wakimfahamu na kupata hifadhi ya chakula kwa watu wachache waliokuwa wakikumbuka fadhali zake.
Baada ya maisha ya kuhangaika katika Jiji la Nairobi, hakuweza tena kusakata soka, hivyo alianza kujiingiza katika maisha ya uhalifu baada ya kujiunga na makundi ya baadhi ya wenyeji.
Fashanu aliishi kwa muda mrefu katika kitongoji cha Majengo na kufanya uhalifu hatimaye alikuwa na tabia ya kwenda kujificha katika kitongoji cha Dandora kilichoko Kaskazini Mashariki mwa Jiji la Nairobi kikiwa umbali wa kilometa kumi na mbili hadi kumi na tano kulingana na njia itakayoitumia.
Kutoka katikati ya Jiji la Nairobi inaweza kukuchukua takribani dakika ishirini hadi arobaini na tano kutokana na hali ya msongamano wa magari.
Dandora ni makazi ya takriban watu milioni moja wanaoishi katika mitaa duni ya eneo hilo. Ni eneo mojawapo linalotumiwa kutupwa uchafu kutoka katika Jiji la Nairobi na pia ni eneo maarufu kwa watu wanaojihusisha na biashara ya ya takataka.
Uvundo unaotoka kwenye taka ni mkali sana unaweza kukutia uchizi. Hali huwa inakuwa mbaya zaidi pale mvua inaponyesha. Wenyeji walikuwa na msemo wao hakuna kitu chochote kizuri kilichokuwa kinaweza kutoka Dandora.
Baadhi ya vijana wa eneo hilo, wanaishi kwa kuchokonoa takataka wakikusanya vifaa kisha kwenda kuviuza katika viwanda vya plastiki.
Wengine wakajiunga na magenge ya uhalifu ilimradi kuzitafutia familia zao riziki. Familia nyingi zinaishi kwa kipato cha chini ya dola moja. Fashanu alikuwa akiishi katika kibanda kimoja kilichokuwa jirani kabisa na dampo la kutupia takataka.
Ndani ya chumba alichokuwa akiishi hakukuwa na umeme wala kitu chochote cha thamani zaidi ya magodoro yaliyochakaa na mifuko aina ya viroba iliyogeuzwa kuwa mashuka.
Ndani ya chumba harufu ya uvundo ilitawala lakini iliweza kudhibitiwa kidogo na harufu ya bangi zilizokuwa zikivutwa na Fashanu pamoja na vijana wengine waliokuwa wakiishi pamoja naye.
Baada ya mwenyeji aliyekutana naye kuwasiliana na watu kadhaa, hatimaye Muddy alipewa simu na kuzungumza na Fashanu.
“Haloo…” Muddy alisema.
“Fashanu hapa, nani mwenzangu?”
“Muddy Manyara wa Dar es Salaam, Gerezani…”
“Aaaah Mtoto wa Mjini…?”
“Naam ndiye miye swahiba…”
Mawasilino hayo yalifanikisha wawili hao kuonana baada ya Fashanu kutoa maelekezo kwa vijana wake kumfuata Muddy Majengo na kumpeleka Dandora.
Ilikuwa ni furaha kubwa kwa Fashanu kukutana na Muddy ambaye alikuwa jirani yao Gerezani.
***
Pamoja na kumwamini Fashanu lakini Muddy alichukua taadhari na kumficha baadhi ya mambo. Hakutaka kufunguka kila kitu kwa jamaa yake.
Mazingira yalimtisha na kuamini jamaa yake hakuwa tena mtu wa kawaida kama ambavyo alivyokuwa akimfahamu walipokuwa wakiishi pamoja Tanzania.
Hivyo, Muddy hakutaka kumwambia ukweli alikozipata pesa zilizomfanya kufunga safari hadi Nairobi ili kukamilisha safari yake ya kwenda kuishi Ulaya.
Mbali na kutotaka kumwambia kiasi halisi alichokuwa nacho, pia hakutaka kumwambia ukweli wa tukio alilokuwa amelifanya Kariakoo mara baada ya kukutana na Mkongomani, Kamba Makambo.
Hata hivyo, alishindwa kumficha Fashanu kwamba pesa hizo amezikwapua, lakini hakutaka kuzama kwa undani zaidi na hata kiasi pesa hakukitaja kwa ukamilifu.
Muddy alimuonesha Fashanu kiasi kidogo cha fedha huku kingine akikificha kwa kuhofia kufanyiwa kitu mbaya na jamaa yake huyo.
Hakutaka kumwamini kwa asilimia mia moja, ingawaje alikuwa akimtegemea kwenye mipango yake ya kutaka kufika Ulaya.
Pia, hakutaka kuwaamini marafiki wa Fashanu kina Omondi, Kimathi, Njuguna, Jonh na wengine ambao sura zao zilionekana kuwa tayari kufanya jambo lolote ili mradi kupata pesa katika kuendesha maisha ya kila siku.
Marafiki hao wa Fashanu walishanusa harufu ya pesa baada ya kumuona Muddy lakini hawakuwa na ubavu mbele ya mwenyeji wake, walikuwa wakimuogopa Fashanu kutokana na ubabe wake.
“Nikajua Mtoto wa Mjini umeuza nyumba…?” Fashanu alizidi kumdodosa Muddy.
“Hapana niliendeleza harakati tu…ng’ombe mmoja aliingia ndani ya kumi na nane zangu, nikampasua maini,” Muddy alidanganya na kumfanya Fashanu kuangua kicheko.
Fashanu alimpokea rafiki yake, kwani alitegemea kwa siku chache atakazokuwa amekaa naye maisha yake yangebadilika kutokana na kuweza hata kubadilisha mlo kwa siku mbili tatu.
Pia, alijua asingeweza kukosa chochote kitu, hata kama kidogo kutokana na msaada ambao angempa Muddy kwenda kutafuta maisha ughaibuni..
“Nitakutengenezea njia nzuri ya kwenda Uholanzi,” Fashanu alimwambia baada ya Muddy kumweleza lengo ya safari yake.
“Sawa…”
“Mchongo utakaokupeleka kule ni kwenda kusoma, lakini ukifika Amsterdam wewe mwenyewe itakuwa akili kichwani mwako…kajichanganye mitaani na uanze kutafuta maisha yako.
“Kikubwa ukifika Ulaya unatakiwa kuwa mvumilivu… unaweza hata kulala mtaani ukajifunika maboski… huku ukitafuta kazi ya uhakika,” Fashanu alimsisitiza.
“Sawa, ndio maana nilikutafuta wewe,” Muddy alionesha kumkubali rafiki yake na kumwambia kuhusu ujio wa Hamisi.
“Naye anataka kwenda Ulaya?”
“Nilitaka kuondoka naye lakini nadhani pesa haitatosha, hivyo anaweza kubaki hapa.”
“Basi muache aje kushangaa Nairobi, si unajua hii ni Ulaya ndogo!” alisema Fashanu ambaye alimwambia Muddy kwamba alikuwa akifahamihamiana na baadhi ya watu ambao wangehitaji pesa kiasi ili kufanikisha mpango wake.
“Hakuna shaka ilimradi mchongo uende vizuri…” Naye alimhakikishia Fashanu kwamba mambo yakiwa sawa, watagawana kilichokuwapo.
Siku chache baada ya kufika Nairobi, mipango ya kuhangaika safari ya Uholanzi ilianza. Ilimbidi Muddy kumsubiri Fashanu katika geto la Dandora wakati alipokuwa akienda mjini kukutana na baadhi watu wanaojua jinsi kutengeneza mipango ya kusafiri kwenda nchi za Ulaya.
Fashanu alimhakikishia Muddy watu aliokuwa akikutana nao kusuka mipango hiyo walikuwa mahiri sana kwa kutengeneza mipango.
Pia, akamtaka asiwe na wasiwasi kwa sababu ameshafanya kazi nyingi chafu na watu hao na wengi walifanikiwa na hadi wakati huo walikuwa wakiishi Ulaya.
“Kitu feki kinakuwa halali na halali kinaweza kuwa feki, hivyo usiwe na wasiwasi jamaa ni mafundi sana…” Fashanu alimhakikishia Muddy.
Kitu kimoja kilimkera sana Muddy, Hakupenda kuishi Dandora. Mazingira yalikuwa magumu sana lakini ilibidi kukubali na kuvumilia hali hiyo ili kuweza kupata nafasi ya kwenda kufanya shughuli zake Ulaya.
Kabla ya kuyakubali maisha ya Dandora, Muddy alikataa kuishi katika mazingira hayo, alitaka kwenda kutafuta hoteli mjini lakini Fashanu alimkatalia.
“Utapotea mapema sana… kwanza pesa uliyokuwa nayo ni ndogo…itaishia kuwahonga mapolisi…” alimwambia na kumsisitizia maaskari wa Kenya wanapenda sana pesa.
Maelezo ya Fashanu yalimfanya Muddy kuzinduka katika lindi zito la fikra na kuhisi kuwa alikuwa na kesi ya wizi alikotoka, hivyo alihisi askari wa Tanzania wangeweza kumfuatilia hadi Nairobi.
Kutokana na fikra hizo, aliamini hadi kufikia hapo bado hakuwa katika mikono salama, kwani lolote lingeweza kutokea.
Siku nne baada ya Muddy kuingia Nairobi, Hamisi naye aliingia jijini humo. Kama ilivyokuwa desturi, naye alianza kumtafuta Fashanu katika maeneo ya Majengo hadi akafikishwa Dandora.
Yeye hakupata tabu sana kwa kuwa kulikuwa na taarifa za kufika kwake. Hivyo, alivyofika Majengo na kujitambulisha kwamba alikuwa mgeni wa Fashanu alipokelewa na kupelekwa Dandora.
“Mbona umechelewa sana?” Muddy alimhoji baada ya wawili hao kujitenga peke yao na kuanza kupiga stori kuhusu mambo yaliyotokea Tanzania baada ya Muddy kufanya tukio. Hawakutaka mazungumzo yao yasikike na watu wengine.
“Nilichelewa kupata passport…” Hamisi alijitetea.
“Hukumuona Aisha?” Muddy alimuulizia dada ambaye walikuwa wakimfahamu katika Jeshi la Uhamiaji na aliyekuwa msaada mkubwa kuweza kupata hati yake ya kusafiria.
“Hakuwepo, niliambiwa alikuwa ameenda likizo.”
“Kwahiyo ikawaje?”
“Ilinibidi kuzunguka mbuyu ili kuweza kufanikisha kuipata…”
“Haya nipe michapo ya huko nyumbani…”
“Baada ya siku mbili tu ile gari uliyoiacha kule Kongowe ilitangazwa kwenye tv, magazeti na vituo vya redio…” alianza kuhadithia Hamisi na Muddy akiwa na hamu ya kusikiliza kuhusu taarifa hizo.
Inaendelea…