
Tom Barrack, balozi wa Marekani nchini Uturuki na mjumbe maalumu wa masuala ya Syria, ametoa onyo la kutisha kwa Lebanon akiitaka ama iipokonye silaha Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya nchi hiyo Hizbulla au ikabiliwe na mashambulizi mengine ya Israel na migogoro ya kiuchumi na kisiasa.
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii, Barrack amesema: “ikiwa Beirut itashindwa kuchukua hatua, mkono wa kijeshi wa Hizbullah bila shaka utakabiliwa na makabiliano makubwa ya Israel wakati Israel iko kwenye hali ya nguvu ilizonazo wakati huu, huku Hizbullah inayoungwa mkono na Iran ikiwa katika hali dhaifu zaidi”.
Mjumbe huyo wa Marekani ameendelea kudai kwamba, Hizbullah inaweza kushinikiza uchaguzi wa Bunge la Lebanon uakhirishwe mnamo Mei 2026 ikiwa vitatokea vita wakati huo na kushadidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.
Barrack amesema msukumo wa Beirut wa kuvifanya vikosi vya ulinzi vya Lebanon viwe nguvu pekee ya kijeshi nchini humo ungali uko zaidi kwenye hali ya matarajio kuliko ukweli halisi kutokana na kile alichokiita mamlaka ya utawala wa kisiasa ya Hizbullah na “hofu ya machafuko ya ndani”.
Mwanadiplomasia huyo wa Marekani ameendelea kutoa matamshi ya kuingilia masuala ya ndani ya Lebanon katika hali ambayo, Harakati ya Hizbullah kupitia Katibu wake Mkuu Sheikh Naim Qassem imeshasisitiza mara kadhaa kwamba, watu wa Lebanon na Muqawama kamwe hawatakubali kudhalilishwa au kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na adui mzayuni, na kwamba njia yao itaendelea kubaki kuwa ya Imam Hussein iliyokita mizizi katika heshima, kutokubali kudhalilishwa na kujitolea muhanga…/