Raila Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC News Swahili

Kifo cha Raila Amolo Odinga mnamo Oktoba 15, 2025, kimeiweka chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika wakati mgumu.

Odinga, ambaye aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80 nchini India, kutokana mshtuko wa moyo, alikuwa mwanzilishi wa chama, na alitambuliwa kuwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya na kigogo wa mageuzi ya kidemokrasia.

Kutokuwepo kwake kunazua maswali muhimu kuhusu uwiano, uongozi na umuhimu wa chama cha ODM wakati Kenya inapoelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Wachambuzi wanasema hatua ya chama hicho kuegemea chapa ya kibinafsi ya Odinga kunakiweka hatarini ikizingatiwa jinsi hali ya kisiasa inavyobadilika kwa kasi.

Urithi wa Raila Odinga

a

Chanzo cha picha, Odinga

Ushawishi wa Raila Odinga ambaye alikuwa kiongozi mwanzilishi wa ODM, haukuwa na kifani.

Alikuwa na uungwaji mkono katika maeneo ya Nyanza, Magharibi mwa Kenya, na baadhi ya maeneo ya mwambao wa Pwani, akigombea urais mara tano kati ya mwaka 1997 na 2022. Utetezi wake wa demokrasia ya vyama vingi na mageuzi ya katiba, hasa Katiba ya 2010, uliimarisha jukumu la chama cha ODM kama nguvu ya mageuzi katika siasa za Kenya.

Hata hivyo, uongozi wa Raila pia ulikifanya chama kutegemea mwelekeo aliotoa kisiasa, huku viongozi wakuu wa chama mara nyingi wakizingatia mamlaka yake.

Migawanyiko ya ndani ilikuwa tayari imeanza kujitokeza hata kabla ya kifo chake. Mnamo Oktoba 2024, mvutano uliibuka kuhusu kuteuliwa kwa Gavana wa Kisumu Peter Anyang’ Nyong’o kama kiongozi wa muda, huku baadhi ya viongozi wakuu wakihoji hatua ya Odinga kuunga mkono serikali na umri wake.

Wiki kadhaa kabla ya kifo chake Rail lisema: ”Sisi ni ODM. Nani alikuambia kuwa ODM haitakuwa na mgombea 2027? Tuna mpango wa wazi ambao tumejadiliana na kuafikiana. Tuendelee kutekeleza mpango huo. Maamuzi mengine yatachukuliwa wakati utakapofika”.

Wakati wa ibada ya mazishi yake huko Bondo magharibi mwa Kenya Jumapili tarehe 19 Oktoba viongozi kadhaa wa ODM walionekana kutofautiana hadharani kuhusiana na hatma ya chama hicho.

Mizozo hii inaangazia changamoto pana inayokabili ODM katika kudumisha umoja bila uwepo wa Raila Odinga. Katika miji ya Kisumu, Migori, Siaya, na Homa Bay, wakaazi ambayo ni ngome kuu ya kisiasa walimtaja Raila kama “mfalme” na kuonyesha wasiwasi juu ya uwezekano wa kutengwa kisiasa, kuashiria ugumu wa chama kudumisha uungwaji mkono wake kijamii na kitaifa.

Changamoto ya uongozi na utambulisho

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya marehemu Raila Odinga

Chanzo cha picha, Raila Odinga/Facebook

Ingawa Seneta wa Siaya Oburu Odinga ameteuliwa kuwa Kaimu Mwenyekiti wa chama baada ya kifo cha kaka yake Raila Odinga suala ambalo linastahili kushughulikiwa haraka iwezekanavyo ni lile la uongozi.

Hakuna kiongozi hata mmoja, anayeonekana kufikia hadhi ya kitaifa ya Raila Odinga. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba uwezo wa chama kumpata kiongozi atakayeunganisha wafuasi na mwenye haiba kubwa utaamua mustakabali wake katika chaguzi zijazo.

Kifo cha Raila huenda kikazua malumbano ya kisiasa na kusababisha mpasuko wa ndani ikiwa pande zinazotofautiana mirengo zitashindwa kuungana kwa maslahi ya chama.

Uhusiano wa ODM na serikali ya Rais William Ruto pia huenda ikatatiza muelekeo wa chama kuenda mbele. Ushirikiano wa hivi majuzi kati ya Odinga na Rais Ruto, ikiwa ni pamoja na mchango wa ardhi kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu wa Ruto mjini Kisumu mnamo Mei 2025, uligubika utambulisho wa chama hicho cha upinzani.

Wakati Raila alishikilia kuwa ODM haikuwa sehemu ya serikali, uamuzi wake ulizua sintofahamu miongoni mwa wanachama na wafuasi wa chama, haswa uchaguzi wa 2027 unapokaribia. Viongozi chipukizi ambao wana ukuruba na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) huenda wakadhoofisha chama cha ODM.

Shinikizo kutoka nje

,

Chama cha pia kinakabiliwa na ushindani wa nje. Wapinzani wake kama vile aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka wamekuwa wakipinga ubabe wa ODM huku baadhi ya wabunge akiwemo Caroli Omondi wa Suba Kusini wakionya kuhusu kupungua kwa ushawishi katika ngome za jadi.

Kushindwa kwa Raila katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mapema mwaka wa 2025 pia kulidhihirisha udhaifu katika wasifu wa chama kitaifa na kimataifa.

Licha ya changamoto hizi, mfumo wa kitaasisi wa ODM na umuhimu wa kihistoria inaipatia msingi wa uthabiti. Jukumu lake kuu sasa kutengeza mazingira ya kidemokrasia ya Kenya na mitandao yake dhabiti wa uwakilishi ya kitaifa unaipatia fursa mpya.

Wachambuzi wa mambo wanadokeza kwamba chama hicho lazima kinadi upya utambulisho wake, kiimarishe uongozi mpya, na kuweka wazi msimamo wake wa upinzani huku kushughulikia migawanyiko ya ndani na shinikizo kutoka nje.

Urithi wa Raila kama mwanademokrasia na mwanamageuzi utaendelea kutoa hamasa, lakini mustakabali wa chama hicho utategemea uwezo wake wa kusonga mbele ya baada ya enzi ya Raila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *