Mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner, ambaye ni mmoja wa wapatanishi wake wakuu katika mpango wa kusitisha mapigano Ghaza, amesema harakati ya Palestina ya Hamas imekuwa “ikitekeleza kwa nia njema” makubaliano hayo, akiashiria taarifa zilizopokelewa kutoka kwa wapatanishi wa kikanda waliohusika katika mazungumzo ya usitishaji huo wa vita.

Akizungumza katika mahojiano yaliyorushwa hewani jana Jumapili kwenye kituo cha televisheni cha CBS, Kushner alisema Marekani, Israel na wapatanishi wanafuatilia kwa pamoja utekelezaji wa makubaliano hayo, ikiwa ni pamoja na kufanikisha kuachiwa huru mateka wa Israel na mabaki ya maiti za mateka hao yanayoshikiliwa na Hamas huko Ghaza.

“Kwa mujibu wa tunavyoona kutokana na kile tunacholetewa kutoka kwa wapatanishi, wako hivyo hadi sasa,” alijibu mkwe huyo wa Trump alipoulizwa kama Hamas inaheshimu makubaliano hayo.

“Hilo linaweza kuvunjika wakati wowote, lakini hivi sasa, tumewaona wakionyesha kuheshimu makubaliano waliyofikia.”

Kushner, ambaye pia kwa sasa anahudumu kama mshauri asiye rasmi wa serikali yaTrump, amesema Washington “inashinikiza pande zote mbili (za Israel na Hamas) kuwa makini katika kutafuta suluhu badala ya kulaumiana kwa kuvunjika makubaliano”, akisisitizia lengo la kudumisha utulivu wakati awamu ya kwanza ya usitishaji vita inaendelea.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mamlaka za Palestina katika Ukanda wa Ghaza zimetangaza kuwa, tangu yaliposainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano hadi sasa, jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limefanya mashambulizi kadhaa ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 97 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 230.

Kwa mujibu wa mamlaka hizo, katika kipindi hichom jeshi la utawala ghasibu wa Israel limekhalifu makubaliano hayo ya kusitisha vita mara zisizopungua 80, ukiwa ni ukiukaji wa wazi wa azimio la usitishaji mapigano na sheria ya kimataifa ya kibinadamu…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *