Nahodha na mshambuliaji wa kikosi cha wakubwa cha Argengina, Lionel Messi, ametuma ujumbe wa kuwafariji wachezaji wa timu ya taifa hilo chini ya miaka 20, baada ya kupoteza mechi ya fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco.
Jana Jumapili, Oktoba 19, 2025, kikosi cha Argentina chini ya miaka 20 kilipoteza mechi ya fainali kwa kufungwa 2-0 na Morocco, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nacional Julio Martínez Prádanos nchini Chile.
Messi, ametuma ujumbe huo wa kutia moyo kwa kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 cha Argentina, baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Morocco kwenye mechi ya fainali.
Baada ya kipigo hicho, Messi alichapisha ujumbe wenye hisia kwenye ukurasa wake wa Instagram Story, akionesha fahari na kuwaunga mkono vijana waliowakilisha taifa hilo kwenye fainali za vijana chini ya miaka 20.

“Mmepambana sana vijana! Mlikuwa na mashindano mazuri sana, japokuwa tulitamani kuwaona mkilibeba kombe, tumebaki na furaha ya kila kitu mlichotupa na fahari ya kuwaona mkiitetea jezi ya bluu na nyeupe kwa mioyo yenu yote,” ameandika Messi.
Katika mechi hiyo ya fainali, mabao mawili ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Yessir Zabiri yaliipa Morocco ushindi na kuiweka historia kama taifa la pili kutoka Afrika kutwaa taji hilo, baada ya Ghana kufanya hivyo mwaka 2009.
Argentina ilikuwa na kampeni nzuri kuelekea mechi ya fainali, ikiwa ni moja ya timu mbili pekee zilizoshinda mechi zote za hatua ya makundi. Katika hatua za mtoano, iliendelea kung’ara kwa kutofungwa bao hata moja, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 4-0 dhidi ya Nigeria katika hatua ya 16 bora.
Ingawa Argentina ilimiliki mpira kwa kiwango kikubwa katika fainali hiyo, Morocco iliwazidi kiufundi na kutumia vyema makosa ya vijana wa kocha Diego Placente.

Historia ya Argentina kwenye Kombe la Dunia U-20
Argentina ndio taifa lenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya fainali za Kombe la Dunia chini ya miaka 20, ikiwa imelitwaa taji la michuano hiyo mara sita, ikiwa ni rekodi ya juu zaidi, pia ndio timu pekee iliyowahi kulibeba mara mbili mfululizo.
Kwa upande mwingine, Lionel Messi mwenyewe aliwahi kuiongoza Argentina kubeba taji hilo mwaka 2005, akifunga mabao mawili kwenye fainali waliyoshinda kwa 2-1 dhidi ya Nigeria.