
Hivi karibuni hatua ya makundi ya mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa upande wa Bara la Afrika ilifikia tamati.
Kukamilika kwa hatua hiyo kulifanya idadi ya timu tisa ambazo zinafuzu moja kwa moja kuiwakilisha Afrika katika Fainali hizo za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Marekani, Canada na Mexico kukamilika rasmi.
Timu hizo tisa za taifa ambazo zitapeperusha bendera ya Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia ni Morocco, Algeria, Tunisia, Ghana, Misri, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Senegal.
Mambo hayakuenda vizuri kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo katika kundi lake lililokuwa na timu za Morocco, Niger, Zambia na Congo ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi tisa.
Jambo ambalo halifurahishi zaidi ni kwamba Taifa Stars ilimaliza hatua hiyo kwa kutopata ushindi katika mechi nne mfululizo za mwisho ambazo moja ilitoka sare na Congo huku ikipoteza michezo mitatu dhidi ya Morocco, Niger na Zambia.
Ikumbukwe pia Taifa Stars iliishia katika hatua ya robo fainali ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) 2024 ambapo ilifungwa na Morocco.
Hilo limepelekea kuwepo na lawama nyingi zinazoelekezwa kwa benchi la ufundi ambalo kundi fulani la wadau wa soka nchini linaamini limeshindwa kuiongoza timu hiyo.
Hata hivyo kama nchi tunatakiwa kufahamu sababu ambazo zinachangia kuifanya Taifa stars isipate mafanikio makubwa katika jukwaa la kimataifa na kuamua kutafuta suluhisho la pamoja badala ya kutafuta watu fulani wachache na kuwanyooshea kidole.
kwa hali ilivyo sasa, kunyooshea kidole kundi fulani la watu sio sahihi kwa sababu kama taifa hatuonekani kuwa na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha tunakuwa na timu imara ya taifa ambayo itatutoa kimasomaso katika mashindano ya kimataifa.
Sera na mipango ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiandaa inaonekana kwenda tofauti na ile iliyopo katika klabu zetu nyingi ambazo zenyewe ndio zinategemewa zitoe wachezaji wa kwenda kuitumikia timu ya taifa.
Mfano, kwa sasa TFF inaendesha ligi za vijana kwa umri wa miaka 17 na 20 lakini tunashuhudia klabu nyingi zikitumia wachezaji ambao wamevuka umri lakini hata matunzo ya vikosi hivyo vya vijana sio mazuri.
Lakini pia kundi kubwa la wachezaji wetu wa Kitanzania, wamekuwa hawajitumi katika klabu zao jambo ambalo limekuwa likipelekea zitoe fursa kwa wachezaji wa kigeni.
Kwa hali hii ya pande husika katika soka nchini kutoonyesha muelekeo wa pamoja, tusitegemee kama tutakuwa na timu imara ya taifa.
Hizo nchi zote zinazofanikiwa, watu wake wa soka wanazungumza lugha moja.