Dar es Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Yanga chini ya Rais, Hersi Said imeanza haraka mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu mpya, muda mfupi baada ya kuachana na Romain Folz.

 Yanga iliamua kumtupia virago Romain Folz, baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Silver Strikers ya Malawi kwa bao 1-0.

 Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga ni kwamba klabu hiyo haitaendelea na hesabu za kumchukua Romuald rako-tondrabe kutoka Madagascar ambaye awali alitajwa kuwa ndio atakuwa mrithi wa Folz na sasa inasaka kocha mwingine.

Bosi mmoja wa juu ameliambia gazeti hili kuwa, mchakato wa Roro hautaendelea kufuatia uongozi wao kuachana naye kwa sababu ambazo hata hivyo hawakutaka kuziweka wazi.

“Ni kweli tulikuwa na hesabu za kumchukua kocha Rakotondrabe (Roro) lakini kuna mambo yametupa wasiwasi. Hatutaweza kuendelea na huo mpango tena.

“Tutarudi kuanza mchakato upya kabisa, tunataka kufanya mambo kwa umakini zaidi, tupate kocha ambaye atatupa kile ambacho tunakitarajia kama klabu,” alisema bosi huyo.

Folz ameiongoza Yanga kwenye mechi sita za mashindano akishinda nne, akitoa sare moja na kupoteza moja. Chini yake, Yanga imefunga mabao tisa huku bao pekee ilililoruhusu juzi, ndio likaitimisha maisha yake ndani ya klabu hiyo, akichukua taji moja la Ngao ya Jamii.

Timu hiyo Sasa itakuwa chini ya kocha Patrick Mabedi aliyekuwa msaidizi wa Folz wakati Yanga ikitafuta kocha mpya wa kuja kuendelea na majukumu ya kukinoa kikosi hicho.

Kocha wa zamani wa Yanga Nasreddine Nabi ameitaka Yanga kuwa makini kwenye mchakato wa kupata kocha mpya akisema wanahitaji kocha mwenye ufundi wa kisasa utakaoiruhusu timu kujenga mashambulizi.

Nabi ambaye ni kocha wa zamani wa timu hiyo, alisema hana shida na ubora wa wachezaji wa kikosi hicho lakini akasema inahitaji kocha ambaye ataweza kuwalazimisha wachezaji kujituma na kutekeleza ipasavyo yale ambayo ya-natakiwa na kocha huyo.

“Sio taarifa nzuri kwa Yanga kupoteza kocha wakati huu. Kuna presha inaongezeka kwa uongozi na hata timu lakini naamini wanaweza kurudi kwenye utulivu siku zote naamini hatua zao.

“Nilikuwa hapo Tanzania, niliwaona (Yanga). Sina tatizo na ubora wa wachezaji wao hata kocha lakini nadhani wanahitaji kocha mwenye uzoefu mkubwa anayeweza kuisimamia klabu yenye presha ya matokeo kama Yanga.

“Nilivyowaona ni kama wachezaji walikuwa hawaogopi kucheza nje ya maelekezo, wanahitaji kocha ambaye akiwa nje amesimama wachezaji wake watakuwa wanakumbuka kile wanachotakiwa kufanya,” alisema Nabi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *