Ijumaa ya Oktoba 11 mwaka huu jijini London kulikuwa na mechi ya soka ya wakongwe wa Chelsea dhidi ya wa Liverpool dimbani Stamford Bridge. Ilikuwa mechi nzuri iliyorudisha kumbukumbu ya miaka zaidi ya 10 iliyopita.

Liverpool walishinda 1-0 kwa bao la mdachi Ryan Babel ambaye alilitoa kwa Diogo Jota kama heshima….kupitia ush-angiliaji wake wa papa mtoto. Kulikuwa na matukio mengi lakini kubwa zaidi ni vita vya mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa dhidi ya beki wa Liver-pool Martin Skrtel.

Kama mechi ililenga kuleta hisia za zamani, basi hawa jamaa walifanya ilivyostahili zaidi. Dakika ya 30, Martin Skrtel alimfanyia madhambi Costa, naye kama kawaida huwa hanaga unyonge…akasimama na kutanua mbavu kibabe.

Akamrukia beki huyo raia wa Slovakia na kutaka ‘kumfanya vibaya’ kabla ya kuamuliwa na wachezaji wa pande zote. Dakika chache baadaye Diego Costa akalipa yale madhambi na kupata kadi ya njano.

Huyu ndiye Diego Costa halisi…Diego Costa yule yule aliyekuwa akipigana uwanjani kila mechi kama mbwa aliyekula pilipili kichaa. Ugomvi huu dhidi ya Martin Skrtel ulirudisha kumbukumbu halisi za miaka ya zamani baina ya timu hizi.

Japo Chelsea na Liverpool sio watani wa jadi, lakini vita vya mataji vilieagombanisha kuanzia katikati ya miaka ya 2000 na kugeuka kuwa maadui na mechi yao kuwa ya ushindani kweli kweli.

Goli la mizimu (Ghost Goal) la Luis Garcia wa Liverpool dhidi ya Chelsea kwenye nusu fainali ga ligi ya mabingwa 2005 ndio hasa vita ilipoanzia. Matukio ya kibabe baina yao yakawa ya kawaida…na ndicho kilichotokea kwa wakongwe hawa.

Vita binafsi baina yao ilianza Januari 27, 2015 dimbani Stamford Bridge kwenye mechi ya kombe la Carabao. Diego Costa alimtimba Martin Skrtel aliyekuwa ameanguka chini, na kusababisha ugomvi mkubwa baina yao.

Wakavimbiana na kukunjana…kama walivyofanya kwenye mechi ya wakongwe. Baada ya mechi Costa akashitakiwa na chama cha soka FA kwa kosa hilo na lingine kama hilo dhidi ya Emre Can kwenye mchezo huo huo…akafungiwa mechi tatu.

Novemba mwaka huo huo kwenye mchezo wa ligi kuu, Costa alimkanyaga tena Skrtel, safari hii kifuani, wakati wote wakiwa wameanguka. Mwamuzi wa mchezo huo, Mark Clatternburg aliliona tukio na kulichukulia hatua pale pale.

Hii ndio ilikuwa pona yake kwani ingebainika mwamuzi hakuona, basi angeshitakiwa na kamati na hukumu yake ingekuwa si chini ya mechi nne. Costa aliondoka Chelsea 2017 lakini bado hajastaafu rasmi kusakata kabumbu…japo hana timu kwa sasa.

Akiwa na miaka 37 sasa, muonekano wake ni ule ule wa miaka 10 iliyopita alipokuwa na miaka 37. Wakati ule muonekano wake ulikuwa wa kiutu uzima kuliko umri wake na kuibua tetesi kwamba labda kadanganya umri.

Lakini miaka 10 baadaye bado anaonekana vile vile, huku wengine wote wakiwa wamebadilika…wamezeeka! Yawezekana yeye alikuwa mbele ya muda…alikuwa miaka 10 mbele.

Lakini ukorofi wake bado uko pale pale…bado ule ule.

Diego Costa ni mshambuliaji mkorofi sana, sio tu kwa matendo ya uwanjani bali hata kauli za ushuhuda kutoka kwa wa-tu wa karibu. Wakati akijiunga Chelsea mwaka 2014, alimfuata nahodha John Terry na kumwambia.

“Naenda kwenye vita. Ungana na mimi.” Na kweli,  kwa Diego Costa kila mechi ilikuwa vita.  Alipambana na wapinzani, alipambana na waamuzi na hadi mashabiki wa timu pinzani.

Maadui walimchukua…mamlaka za soka zilimhukumu lakini mashabiki wa timu yake walimpenda.

MZEE WA FACT: Kuna vitu havibadiliki anawatisha mabeki wa timu pinzani na kuwatia hofu. Mechi dhidi ya timu ya Diego Costa ilikuwa mechi kweli kweli. Hakuna beki angependa akutane na jamaa.

Miaka 10 baada ya matukio yake ya kibabe dhidi ya Liverpool,  amerudi Stamford na kufanya vile vile, dhidi ya yule yule kwenye mechi ile ile na uwanja ule ule. Kuna vitu huwa havibadiliki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *