‎‎Dar es Salaam. Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu leo inaendelea kuunguruma  Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam baada ya mapumziko ya mwisho wa juma.

Katika mwendelezo wa usikilizwaji wa kesi hiyo, leo Jumatatu Oktoba 20, 2025, Jamhuri inaanza kujibu hoja za pingamizi la Lissu kuhusiana na upokewaji wa video inayomuonesha akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini, ili iwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”.

Kesi  hiyo  inayosikilizwa na  jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.

Shahidi huyo wa tatu ni Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Eribariki Kaaya miaka (39), Mtaalamu wa picha, kutoka kitengo cha picha kamisheni ya uchunguzi wa sayansi jinai, makao makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.

Kitengo hicho kinajishughulisha na kupinga na kurekodi picha za mnato na za mjongeo za matukio ya uhalifu, watuhumiwa wa uhalifu, na kunafanya uchunguzi wa picha mjongeo, picha mnato.

Hivyo alisema kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kitaalamu katika hatua mbili zilizohusisha uchunguzi wa awali wa kutazama (physical examination) kwa kuzingatia sifa za kitaalamu na  uchunguzi wa kisayansi (forensic examination) alibaini kuwa ilikuwa ni halisi.

Katika ushahidi wake wa msingi akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawab Issa,  shahidi huyo alieleza kuwa  ndiye aliyepokea na kufanyia uchunguzi wa kisayansi video ya Lissu.

Alipokea video hiyo Aprili 8, 2025 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu, Dar es Salaam, moja ikiwa kwenye flash disk na nyingine kwenye kadi ya kuhifadhia data (memory card). 

Shahidi huyo alieleza kuwa baada ya uchunguzi wake huo, alibaini

 na kuthibitisha matokeo ya uchunguzi wa awali, kuwa video hiyo ni halisi.

Hivyo aliandaa ripoti yake ya uchunguzi ambayo pamoja na vielelezo alivyovifanyia uchunguzi alivikabidhi kwa mamlaka iliyoomba uchunguzi huo.

Baada ya kuvitambua vielelezo hivyo akiongozwa na Wakili Issa, shahidi huyo aliiomba mahakama izipokee picha hizo (video) ziwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Hata hivyo Lissu amepinga kupokewa kwa video hizo kuwa kielelezo akibainisha sababu nne.

Sababu ya kwanza amedai kuwa video hizo licha ya kutajwa na kuorodheshwa katika orodha ya vielelezo vya Jamhuri lakini hazikuwahi kuoneshwa katika Mahakama ya Ukabidhi ( Committal Court), katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati wa mwenendo kabidhi (committal proceedings).

Alidai kuwa hilo ni kinyume cha kifungu cha 263(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya Mwaka 2023.

Pia alirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika mashauri mbalimbali akisisitiza kuwa huo ndio msimamo kuwa lazima kielelezo kisomwe au kioneshwe kwanza wakati wa mwenendo kabidhi

Katika sababu ya pili alidai kuwa video hizo zimewasilishwa kabla ya wakati kwani zilipaswa ziwasilishwe baada ya ripoti ya uchunguzi wake kupokewa na ni kinyume na vifungu vya 216 mpaka 220 vya CPA

Katika sababu ya tatu alidai kuwa Shahidi hana mamlaka ya kuziwasilisha mahakamani kuwa kielelezo kwani hana sifa kama mtaalamu wa picha.

Alifafanua kuwa anapaswa kuwa  ameteuliwa kwa jukumu hilo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na atangazwe kwenye gazeti la Serikali (GN).

Hata hivyo amesema kuwa  aliteuliwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye si mamlaka halali na kwamba yeye ni mtaalamu wa picha na si mtaalamu wa uchunguzi wa sayansi jinai.

Katika sababu ya nne Lissu alidai kuwa video hiyo haijajengewa msingi wa mnyororo wa utunzwaji wake tangu ilikopatikana mpaka ilipomfikia shahidi huyo na kuifikisha mahakamani hapo.

 Baada ya Mahakama kupokea hoja hizo za Lissu, iliahirisha kesi hiyo mpaka leo.

Hivyo leo Jamhuri itajibu hoja hizo kabla ya Lissu pia kujibu hoja za Jamhuri na kisha watasubiri uamuzi wa Mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *