Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Dodoma imetoa wito kwa wananchi kuripoti vitendo vya rushwa mapema kwenye vyombo vinavyohusika kwa ajili ya kulinda haki zao na za wengine kwa kutoshiriki wala kuvumilia vitendo vya rushwa.
Aidha, imebainisha kuwa rushwa ni adui wa maendeleo na inapunguza ubora wa huduma za jamii, inavunja haki, inarudisha nyuma maendeleo, inatishia mustakabali wa vizazi vijavyo na kwamba nchi ikiongozwa na uadilifu na umoja, Tanzania itakuwa jamii ya haki, uwazi na maendeleo ya kweli.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 na Naibu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eugenius Hazinamwisho wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea kwenye mbio za Sepesha Rushwa Marathon zilizoandaliwa na Anti-Corruption Voice Foundation (AVF), zinazotarajia kufanyika Novemba 30, 2025 jijini Dodoma.
Hazinamwisho amesema mbio hizo siyo kusanyiko la michezo bali ni jukwaa la kuamsha dhamira, kuunganisha nguvu na kupeleka ujumbe unaogusa mioyo na mapambano dhidi ya rushwa kwamba ni ya watu wote na yanawezekana iwapo watashirikiana.
“Takukuru Mkoa wa Dodoma tumesimama si kama walinzi wa sheria peke yake, bali kama washiriki wa wananchi, tunapambana kulinda rasilimali za umma, haki za kila mtu na utu wa kila Mtanzania na katika mapambano haya ushirikiano kati ya Serikali na jamii ni nguzo muhimu,” amesema na kuongeza kuwa:
“Taasisi hii imekuwa ni mhamasishaji mkubwa katika jamii kupitia kampeni yake ya ‘badili tabia na sepesha rushwa’ na imekuwa chachu kubwa ya uelewa wa vijana, wanawake, viongozi wa dini, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.”

Naibu kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Dodoma, Eugenius Hazinamwisho (katikati) akiwa pamoja na waandaaji wa mbio za Sepesha Rushwa Marathon Jijini Dodoma leo Oktoba 20, 2025. Picha na Rachel Chibwete
Amesema kwa muda mfupi wa kampeni ya sepesha rushwa kumekuwa na matokeo chanya hasa ya uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kuripoti vitendo vya rushwa imeongezeka ambapo kwa sasa wananchi wanaripoti vitendo vya rushwa kuliko ilivyokuwa kawaida.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa AVF, Eliasa Abdalla amesema mbio hizo zilianza rasmi mwaka 2022 ambapo jumla ya watu 700 walijitokeza mwaka 2023 walipata jumla ya washiriki 1,200, mwaka 2024 (1,800) na mbio za mwaka huu wanatarajia kupata washiriki 2,500.
Amesema malengo ya mbio hizo ni kutoa elimu ya rushwa kwa wananchi, maadili na uadilifu na pia ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kupinga rushwa duniani ambayo huadhimishwa Desemba 9 kila mwaka.
Abdallah amesema kwenye mbio za mwaka huu taasisi hiyo itaungana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) ili kutoa elimu ya kujikinga na Ukimwi pamoja na kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani ambayo hufanyika Desemba 1, kila mwaka na kaulimbiu mwaka huu ni “kimbia kwa uadilifu.”
Naye mratibu wa mbio hizo, Zulfa Mselemu amesema AVF imekuwa ikitoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa zilizopo shuleni, vyuoni na maeneo ya kazi ambapo mafanikio ya kampeni hiyo ni makubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.