Shinyanga. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeshauriwa kuanzisha masomo ya amani, uzalendo na mazingira shuleni kuanzia madarasa ya awali hadi vyuo vikuu ili kujengea uwezo wanafunzi kuhusu masuala hayo.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja aliyesema amani, uzalendo na mazingira ni muhimu katika ustawi wa nchi na usalama, akibainisha kuwa watoto wakifundishwa wakiwa watoto wadogo wataweza kuiishi misingi hiyo.

“Utamaduni hauoti kama uyoga, waswahili wanau semi ‘samaki mkunje angali mbichi’, “amesema Mgeja wakati wa mahafali ya kwanza ya darasa la awali na darasa katika shule ya msingi, AL Wahaaab and Primary School.

Katika mahafali hayo yaliyofanyika leo Jumatatu Oktoba 20,2025 wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Mgeja amesema chokochoko zote zinazotokea kote duniani za uvunjifu wa amani na ukosefu wa uzalendo ni tatizo la jamii isiyoandaliwa vyem na kutojua thamani ya amani na uzalendo.

“Bado hatujachelewa kuelimishana umuhimu wa thamani ya amani, uzalendo na mazingira japo kuna viashiria vimeanza kujitokeza kidogo kwa baadhi ya Watanzania wenzetu.

“Wameanza kujaribu kutikisa amani iliyopo, lakini kikundi hicho cha wachache kinajidanganya hakitaweza kuichezea amani kwa sababu nchi yetu iko salama katika uongozi imara wa Samia Suluhu Hassan,” amesema Mgeja.

Kwa nyakati tofauti jeshi la polisi nchini, limekuwa likionya vijana na Watanzania kutojiingiza katika vitendo vitakavyosababisha uvunjifu wa amani, likisema halitamvumilia yeyote atakayebainika.

Katika mahafali hayo, Mgeja amempongeza Rais Samia kwa namna anavyoongoza Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na utulivu, akiwaomba Watanzania kuendelea kumuunga mkono kiongozi huyo.

Mbali na hilo, Mgeja ambaye pia ni mwanasiasa amewapongeza viongozi wa dini kwa kuendelea kuwahamasishwa waumini wao na Watanzania kuitunza amani iliyopo.

Wakurugenzi wa Al Wahaab, Sheikh Mohamed Hilal na Ahmed   Haluna kwa nyakati tofauti wamesema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2019 na imekuwa na mafanikio ikiwemo malezi, elimu na maadili bora.

Sheikh Hilal amesema wamenunua ekari 60 zitakazotumika katika ujenzi ili kupanua shule hiyo, kwa kuweka mabweni, viwanja vya michezo na ujenzi huo utaanza mwakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *