Sean Dyche huenda akatangazwa kuwa kocha mkuu mpya wa Nottingham Forest baada ya mazungumzo kati yake na uongozi wa klabu hiyo kwenda vizuri tangu jana Jumapili jioni Oktoba 19, 2025.
 
Dyche anatarajiwa kuwa kocha mkuu wa tatu katika kikosi cha Forest msimu huu, akitarajiwa kuchukua nafasi ya Ange Postecoglou, aliyetimuliwa juzi Jumamosi Oktoba 18, 2025, kufuatia mambo kumwendea kombo.

Postecoglou alifutwa kazi dakika 18 baada ya Forest kupigwa 3-0 nyumbani na Chelsea. Huku akidumu katika kazi hiyo kwa siku 39.

Dyche, ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa vijana wa Forest, amefanya mazungumzo na mmiliki wa klabu hiyo Evangelos Marinakis na inaelezwa kuwa, yupo tayari kufanya kazi hapo.

Kocha huyo raia wa England, alikuwa chaguo la kwanza, baada ya kuondoka kwa Postecoglou, na alipotafutwa hakusita kuanza mazungumzo na mmiliki Evangelos.

DY 01

Forest ilizingatia mapendekezo mengine ya makocha kama Marco Silva wa Fulham ambaye alikuwa mmoja wa waliokuwa juu kwenye orodha yao. Hata hivyo, Silva atahitaji fidia ya angalau Pauni 8 milioni, ili kuvunja mkataba wake, unaotarajia kumalizika mwakani. 

Mwingine ni Roberto Mancini, aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Italia na Manchester City, pia alishinikizwa na mkuu wa kimataifa wa masuala ya soka Edu Gaspar, lakini mazungumzo hayakuwa na muitikio chanya.

Steve Cooper pia alifikiriwa na Marinakis, lakini shujaa huyo aliyeipandisha daraja Forest mwaka 2022, kwa sasa anaifundisha klabu ya Brondby ya Denmark.

Dyche yupo kwenye hatua za mwisho, na anatarajiwa kuiongoza Forest kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya Europa League dhidi ya FC Porto ya Ureno siku ya Alhamisi Oktoba 23, 2025. Wasaidizi wake wakitarajiwa kuwa wachezaji wa zamani wa Forest, Ian Woan na Steve Stone.

DY 02

Baada ya kumenyana na Porto, Forest itakutana na Bournemouth kisha Manchester United kwenye mechi za Ligi Kuu ya EPL.

Kocha huyo hajaiongoza timu yoyote tangu alipoondoka Everton mwezi Januari 2025. Alifanya kazi katika mazingira magumu sana klabu hapo, ikiwa ni pamoja na kupokonywa pointi mara mbili kwa kukiuka kanuni za kifedha.

Anachukuliwa kuwa kocha anayefaa zaidi kukinoa kikosi cha sasa cha Forest, huku maafisa wakuu wa klabu hiyo wakitamani kuona timu ikirejea kwenye uimara wa safu ya ulinzi ambao ulikuwa silaha kuu chini ya Nuno Espírito Santo.

Dyche aliwahi kuwa mchezaji wa Forest kati ya 1987 na 1990, na kila mara amekuwa akiheshimu mafunzo aliyopata chini ya kocha maarufu Brian Clough.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *