Bayer Leverkusen bado haijapata ushindi katika mechi mbili za awali za hatua ya makundi, wakitoka sare dhidi ya PSV Eindhoven (1-1) na FC Copenhagen (2-2).
Kocha mpya wa Leverkusen, Kasper Hjulmand, ameiongoza timu hiyo bila kupoteza mechi yoyote ndani ya Bundesliga tangu achukue mikoba, lakini bado hajapata ushindi katika michuano ya Ligi ya mabingwa Ulaya.
Leverkusen inakabiliwa na majeraha ya wachezaji muhimu kama Exequiel Palacios, Axel Tape, Malik Tillman, Nathan Tella na Lucas Vázquez.
Kwa upande wao, miamba PSG imeshinda mechi zake mbili za awali, ikiwemo ushindi wa 2-1 dhidi ya Barcelona ugenini.
Katika mechi nyingine, Copenhagen itakutana na Borussia Dortmund katika mechi itakayochezwa kwenye uwanja wa Parken Stadion, Copenhagen.
Copenhagen ilipoteza mechi yao ya awali dhidi ya Qarabağ, na sasa hivi wanahitaji ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano.
Vijana wa Niko Kovac walishinda mechi yao ya awali na wana nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Ekitike arudi nyumbani kuchuana na waajiri wa zamani
Eintracht Frankfurt wataikaribisha Liverpool katika uwanja wa Deutsche Bank Park siku ya Jumatano.
Frankfurt imepata mchanganyiko wa matokeo msimu huu. Waliifunga Galatasaray mabao 5-1 lakini wakapoteza dhidi ya Atlético Madrid.
Na katika Bundesliga mwishoni mwa wiki, walitoka sare ya 2-2 dhidi ya Freiburg baada ya kufungwa bao la dakika ya 87.
Liverpool hata hivyo walianza kwa ushindi wa 3-2 dhidi ya Atlético Madrid japo wakapoteza 1-0 ugenini dhidi ya Galatasaray.
Mshambuliaji Hugo Ekitike aliyejiunga na Liverpool akitokea Frankfurt kwa uhamisho wa pauni milioni 95, anatarajiwa kukutana na klabu yake ya zamani huku kocha Arne Slot akihitaji ushindi ili kurejesha matumaini kwenye kikosi chake.
Kikosi cha Liverpool kimepoteza mechi nne mfululizo katika mashindano yote huku beki wa kati Virgil van Dijk akitoa wito kwa timu kuungana na kuonyesha nidhamu uwanjani.
Mechi hizi ni za mgunguko wa tatu wa hatua ya makundi ya Mabingwa barani Ulaya.