Dar es Salaam. Vuta picha mnakula bata kilabu msha’teketeza pesa za kutosha kwenye pombe na vyakula, na bado pombe zinaendelea kushushwa zikisindikizwa na vibango na ving’ora.

Mara ghafla mshikaji wenu mmoja anasimama na kusema, “mnajua nini wanangu hizi pesa tungefungua biashara tungekuwa tumefanya jambo la maana.” Anawakata stimu. Anaanza kuleta ushauri kwenye bata. Mtu kama huyo Wazungu wanamuita ‘Party Pooper’kwa Kiswahili tungesema mtu anayejisaidia katikati ya sherehe. NAOMBA KUWA PARTY POOPER WA GRAMMY ZA WATANZANIA

Wasanii kadhaa wa Tanzania wameposti kwamba wamepokea ujumbe kwamba ngoma zao zimepitishwa kwa ajili ya kupendekezwa kwenye tuzo za Grammy akiwemo AY na Marioo hilo ni jambo la kupongezwa.

Lakini kwenye mafanikio hayo pia kuna jambo la kukemewa ambalo ni jinsi baadhi ya wasanii hao na vyombo vya habari wanavyoripoti tukio hilo. Wengi wanazungumzia na kuripoti kama vile ngoma za wasanii hao tayari zimechaguliwa kushindania tuzo au tayari zimependekezwa kuchaguliwa kwenye tuzo jambo ambalo ni uongo na upotoshaji usiokuwa na maana.

Sote tunatamani siku moja tuwe na wasanii wenye Grammy Award. Ni fahari kubwa kwa taifa. Lakini hakuna haja ya kuongeza chumvi au kutudanganya Watanzania wenzao. Ukweli ni kwamba Marioo na AY bado hawajachaguliwa wala hata kupendekezwa kuchaguliwa kwenye tuzo hizo. Kilichotokea ni kwamba, kwa sasa wamepokea ujumbe kwamba kazi zao walizotuma zimekidhi vigezo na sasa zinaweza kuingia kwenye hatua ya kupendekezwa. Utaratibu wa Grammy uko hivi.

Hatua ya kwanza msanii anatuma kazi zake pamoja na vipengele anavyotamani kushiriki kwenye tuzo hizo. Grammy wanaripoti kwamba hupokea mamilioni ya nyimbo kutoka kila kona ya dunia. Nyingine hazikidhi hata ubora na vigezo vya Grammy.

Kisha Grammy hutumia muda kuchambua kazi zilizokidhi vigezo na kuwatumia ujumbe wasanii kwamba kazi zao zimekidhi vigezo vya kushiriki tuzo za Grammy. Na huo ndiyo ujumbe ambao Marioo na AY wameupokea.

Hatua ya pili, wasanii waliokidhi vigezo kama AY na Marioo hutakiwa kufanya kampeni za kuwashawishi wapigakura wa Grammy wawapigie kura za mapendekezo. Wapigakura hao au kwa jina lingine ni Recording Academy ni watu ambao wapo kwenye tasnia ya muziki na wengi wao ni kutoka Marekani, nchi ambayo ndiyo waandaaji wa Grammy.

Hatua ya tatu, kazi au wasanii watano kwenye kila kipengele ndiyo huchaguliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Grammy. Msanii akifika hapa sasa ndiyo anaweza hata kujiita msanii wa Grammy maana yake kuwa ‘nominated’ kwenye Grammy ni heshima kubwa.

Naomba nisamehewe kuwa mtu ‘party pooper’, lakini ukweli ni vyema usemwe. Hii tabia ya kutia chumvi imekuwa ikijirudia na siyo kwenye muziki tu hata kwenye filamu. Kwa mfano kuna mwaka flani filamu ilikuwa inatangazwa kuwa ni filamu ya Oscar  tuzo kubwa zaidi za filamu duniani ilihali ilikuwa hata haijachaguliwa bali ilikuwa imechaguliwa na Bodi ya Filamu Tanzania kupitia kamati yake ya tuzo za Oscar kuwa mwakilishi wa Tanzania kwenye tuzo hizo.

Hilo ni somo la siku nyingine, lakini kwa leo tuondoke na somo la kudanganya kuwa tumechaguliwa Grammy hakutatupa Grammy. Tuwahimize wasanii wetu kufanya kazi bora zaidi badala ya kutafuta vichwa vya habari visivyo na ukweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *