LICHA ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, Meneja Mkuu wa timu hiyo, Dimitar Pantev, amesema kikosi chake bado hakijafikia ubora anaoutaka, huku akitamba kutumia mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam kama kipimo cha maendeleo ya timu hiyo.

Mechi hiyo iliyopigwa juzi Jumapili mjini Manzini, Eswatini, ilikuwa ya kwanza ya mashindano kwa Simba chini ya Pantev, ambaye ameanza kazi yake rasmi Msimbazi akirithi mikoba ya Kocha Fadlu Davids.

Ushindi huo umewapa Wekundu wa Msimbazi nafasi kubwa ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwa Pantev, bado hajatosheka anaamini wana nafasi ya kufanya makubwa zaidi hasa katika namna ya kushambulia, kuzuia na kudhibiti mechi.

“3-0 ni matokeo mazuri sana, lakini haimaanishi tumefikia kiwango ninachotaka,” amesema Pantev wakati akizungumza na Mwanaspoti.

PANT 01

“Tunapaswa kujiamini zaidi tutakaporudi Dar es Salaam, kuwa na nidhamu ya kiufundi na kufuata mpango wetu wa mchezo kwa umakini.”

Kocha huyo raia wa Bulgaria, amesema licha ya matokeo mazuri, kulikuwa na upungufu katika namna timu ilivyocheza kipindi cha kwanza, hasa kwenye umiliki wa mpira na mipangilio ya mashambulizi.

PANT 02

“Kuna wakati tuliruhusu wapinzani kuingia katika mchezo kwa sababu tulianza kupiga mipira mirefu kama wao. Tulicheza kwa presha na hilo halikupaswa kutokea,” amesema.

“Wana wachezaji wenye nguvu, hivyo tulipaswa kuwa wavumilivu zaidi na kutumia ubora wetu wa pasi.”

PANT 03

Simba ilionekana kubadilika kipindi cha pili, ambapo maelekezo ya Pantev yalileta matokeo chanya. Kikosi kilicheza kwa kasi, kuumiliki mpira na kutumia vizuri nafasi kati ya mabeki wa kati na wa pembeni wa Nsingizini, jambo lililoifanya kufunga mabao mawili zaidi katika kipindi hicho.

Bao la kwanza lilifungwa kwa kichwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza katika dakika ya 45+2 na beki, Wilson Nangu huku mengine yakifungwa kipindi cha pili na Kibu Denis dakika ya 84 na 90.

“Kipindi cha pili tulicheza kwa akili zaidi. Tulitumia nafasi vizuri, tukashambulia kupitia pembeni na kati. Wachezaji wote walijituma sana, nawapongeza,” amesema Pantev.

PANT 04

“Walionyesha ari na walitaka kupata matokeo. Huo ndiyo moyo ninaoutaka kuujenga ndani ya Simba.”

Hata hivyo, kocha huyo alionya kikosi chake kutoridhika na matokeo hayo akisema ushindi huo ni nusu ya kwanza tu ya kazi na mechi ya marudiano itakuwa kipimo muhimu cha uthabiti wa timu yake.

“Hii ni nusu ya kwanza tu ya kazi yetu. Tunapaswa kuheshimu wapinzani na kucheza kwa umakini ule ule tutakaporudi Dar. Kosa dogo linaweza kubadilisha kila kitu,” amesema.

Simba inatarajiwa kuikaribisha Nsingizini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, katika mechi ya marudiano itakayochezwa Jumapili ijayo Oktoba 25, 2025 na mashabiki wanatarajia kuona timu yao ikimaliza kazi kwa ushindi mwingine.

Tayari benchi la ufundi limeanza mipango kwa ajili ya mechi hiyo, huku Pantev akiahidi kufanya marekebisho machache kwenye kikosi baada ya kurejea nchini ili kuimarisha maeneo ambayo bado hayajamridhisha.

Jana kikosi cha Simba kilitua Dar es Salaam kikitokea Eswatini kukabiliana na Nsingizini ambapo kinajiandaa na mechi ya marudiano kuwania kufuzu hatua ya makundi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *