Serikali ya Donald Trump huko Marekani imevunja rekodi kwa kusimamisha shughuli zake kwa muda wa siku 20. Janga hilo lilianza Oktoba 1, 2025, na kulemaza shughuli muhimu za Marekani na pia kupiga kengele ya hatari ya kuzuka mdororo wa kiuchumi na mgogoro wa kijamii nchini Marekani. Hadi hivi sasa hakuna ishara za kufikia mwisho mgogoro huo wa kisiasa huku mamilioni ya Wamarekani wakiwa chini ya mashinikizo kutokana na maafa ya mgogoro huo kwenye maisha yao.

Shughuli za serikali ya shirikisho la Marekani zimesimama tangu Oktoba 1, 2025 kwa sababu ya kushindwa Baraza la Congress kukubaliana na muswada wa bajeti ya Trump. Hii ni mara ya kwanza kufungwa kazi za serikali kwa muda mrefu zaidi huko Marekani tangu mwaka 2019. Madhara ya kusimamisha shughuli za serikali ni makubwa kwa uchumi wa Marekani na pia kijamii na kisiasa. Mgogoro huu haujavuruga tu maisha ya mamilioni ya Wamarekani, lakini pia kwa mujibu wa Scott Bessent, waziri wa hazina wa Marekani, mgogoro huo unasababisha hasara ya kiuchumia ya dola bilioni 15 kila siku.

Vilevile karibu wafanyakazi 750,000 wa serikali ya shirikisho, wakiwemo wafanyakazi wa Wizara za Ulinzi, Afya na Biashara, wameachishwa kazi bila ya malipo huko Marekani, huku wengine milioni 1.3, wakiwemo wanajeshi na wasimamiaji wa sheria, wakilazimishwa kufanya kazi bila ya malipo. Mgogoro wa kusimamishwa kazi za serikali ulioikumba Marekani mwaka 2019, ulisababisha hasara ya dola bilioni 3 lakini mgogoro wa mara hii kwa mujibu wa waziri wa hazina wa Marekani umeshasababisha hasara ya dola bilioni 300 katika uchumi wa Marekani. 

Utawala wa Trump unatumia fursa hiyo kuwafuta moja kwa moja wafanyakazi katika baadhi ya mashirika ya serikali. Hatua hizo zimezidisha mgogoro wa kifedha, hasa kwa wafanyakazi ambao hawawezi kumudu gharama za maisha kama bima na mafuta.

Huduma za umma zimeingia kwenye matatizo makubwa katika kipindi hiki kigumu huko Marekani. Mbuga za wanyama zimefungwa huku Shirika la Taifa la Utalii la Marekani likiripoti kupata hasara ya dola milioni 20 kila siku.

Askari wa Marekani wakifunga njia ili watu wasiingie kwenye ofisi za serikali kwani huduma zimesimama

Katika sekta ya afya pia, ukaguzi wa ubora wa chakula umesitishwa na hivyo kuhatarisha usalama wa kiafya wa wananchi wa Marekani hasa katika usambazaji wa nyama, maziwa na mayai. Ofisi ya Uhamiaji na Uraia ya Marekani pia imeshindwa kushughulikia maombi ya viza na uraia na hata mipango ya kuwasaidia wahanga wa unyanyasaji wa majumbani imekwama.

Tukija katika usafiri wa anga pia tunaona kuwa nao umekumbwa na uhaba wa vidhibiti vya usafiri na foleni ndefu katika usalama wa safari za ndege. Utoaji wa pasi za kusafiria pamoja na maombi ya mkopo wa nyumba vyote hivyo vimekwama hivi sasa huko Marekani.

Jakamoyo hilo limeikumba pia sekta ya kilimo ambayo ni nguzo muhimu ya kiuchumi. Wakulima nchini Marekani hivi sasa wanayumba vibaya kutokana na kutojua bei za kuuzia bidhaa zao kwani hawapati ripoti za takwimu za bidhaa za kilimo. Mgogoro huo umeyasukuma mashamba 20,000 ya nchi Marekani kwenye ukingo wa shimo la kufilisika kabisa.

Masoko ya fedha nchini Marekani nayo yako chini ya mashinikizo makubwa. Kusimamishwa shughuli za serikali huko Marekani kwa muda wa siku 20 mfululizo kumetoa pigo lisilofidika kwa masoko ya fedha ya nchi hiyo. Kucheleweshwa ripoti ya kila mwezi ya ajira, ambayo ilipaswa kutolewa Oktoba 3, kumeifanya kuwa ngumu kazi ya taasisi za ajira ambazo zimeshindwa kuchukua maamuzi kuhusu viwango vya riba, suala ambalo limeteteresha vibaya soko la hisa.

Biashara ndogo ndogo zinazotegemea kandarasi za serikali pia ziko katika hatari ya kufilisika huko Marekani kutokana na huduma za kugawa kandarasi hizo kukwamishwa na kusimama shughulii za serikali.

Waziri wa Hazina wa Merekani ameonya kwamba kuendelea hali hiyo kunaweza kuusukuma uchumi wa nchi hiyo kwenye mgogoro mkubwa hasa kwa kuzingatia kuwa, ukuaji wa uchumi wa mwaka huu wa 2025 ni dhaifu huko Marekani.

Kwa upande wa kisiasa pia, kusimamishwa shughuli za serikali kumeongeza mivutano na vita baina ya vyama viwili wa Democratic na Republican. Mzozo kuhusu ruzuku ya Obamacare na kupunguzwa bajeti ya Medicaid, ambao ndio uliokuwa msingi wa mazungumzo ya kupitisha bajeti mpya, nao umezidi kuwa mkubwa. Wanachama wa chama cha Democratic wanamshutumu na kumbebesha lawama Trump wakati Warepublican wao wanawalaumu wabunge wa Democratic ambao ni wachache bungeni. Kwa upande mwingine, kura za maoni ya wananchi wa kawaida zinaonyesha kuwa, Wamarekani wengi hawana imani kabisa na taasisi za serikali. Kiwango cha kukubalika utendaji wa serikalii ya Trump kimeporomoka vibaya na kufikia kiwango cha chini kabisa. Wamarekani milioni 24 wanaonufaika na Obamacare wanailaani serikali ya Trump wakisema imewafanya wasiwe salama.

Uharibifu na mgogoro wote huo umekuja huku kukiwa hakuna ishara zozote za kufikiwa maelewano katika Bunge la Congress au kumalizika mgogoro wa kusimama kazi za serikali ya Marekani. Kwa kuzingatia hayo tunaweza kutabiri kuendelea kusimama shughuli za serikali ya shirikisho la Marekani kwa muda mrefu zaidi lakini pia tunaweza kutabiri kuendelea kushuhudiwa hasara za kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata kiusalama nchini Marekani kutokana na mgogoro huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *