
Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Siasa la Hizbullah amesisitiza kuwa, Rais wa Marekani anajiona ni “mtu wa amani” duniani ilhali kiuhalisia yeye ni “mchekeshaji, muigizaji, mdanganyifu na mzandiki, na ndiye gaidi namba moja duniani” aliyemuua shahidi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyed Hassan Nasrullah (Radhi za Allah ziwe juu yake), kwa mabomu ya Mmarekani.
Mahmoud Qamati amesema, serikali ya Lebanon haijawahi kuwepo si wakati wa vita, na si hata wakati wa migogoro na hali ngumu za wananchi, wakati katika nchi nyingine, vita vikimalizika na kuanzishwa usitishaji vita, serikali pamoja na wizara na taasisi zake zote huanza kutoa huduma katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.
Akiihutubu serikali ya Nawaf Salam, Qamati amesema: “mali za wawekaji amana, usambazaji wa umeme, hali ya maisha na utoaji huduma, ahadi zilizotolewa kuhusu kusimamisha uchokozi wa Wazayuni, kuwakomboa mateka na kuyajenga upya maeneo yaliyoharibiwa bila masharti yoyote, yote hayo yamefikia wapi?”
Amasema, badala ya serikali kujaribu kuung’oa mhimili wa nguvu za Lebanon, yaani Muqawama na jeshi, jambo ambalo linaifanya nchi hiyo ikose ulinzi wa kukabiliana na wavamizi, inapaswa ishughulikie majukumu yake ikiwa ni pamoja na kutoa huduma, ili iweze angalau kuheshimiwa na wananchi.
Afisa huyo wa Hizbullah ambaye alikuwa akihutubia hafla ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Mhandisi Reza Avaze na mkewe, Shahidi Masoumeh Karbasi, iliyohudhuriwa na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Beirut na wahusika wengine wa kisiasa na kitamaduni amesema: “Rais wa Marekani Donald Trump anajiona ni “mtu wa amani” duniani, ilhali yeye ni mchekeshaji, muigizaji, mdanganyifu na mzandiki, na ndiye gaidi namba moja duniani” aliyemuua shahidi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyed Hassan Nasrullah (Radhi za Allah ziwe juu yake), kwa mabomu ya Mmarekani, na ndiye aliyeilenga Iran kwa mabomu makubwa zaidi ambayo ni Marekani pekee iliyonayo duniani. Kuko wapi huko kupenda kwako amani na unamdanganya nani? Hakuna amani yoyote. Wao wanataka kutumia jina la amani ili sisi tusalimu amri na kuwatii wao.
Kadhalika, Qamati amezihutubu baadhi ya pande za kimataifa, za kikanda na ndani ya Lebanon, kwa kusema: “msijichoshe bure, sisi hatutasalimu amri mbele ya mashinikizo ya kisiasa na mashambulizi ya kila siku ya Israel”, na akamalizia kwa kusisitiza kwamba, kitakacholeta utulivu nchini Lebanon ni mazungumzo na maelewano ya ndani, na kwamba hilo si jukumu la Muqawama pekee kwa kutoa damu na Mashahidi kwa ajili ya kuilinda ardhi na nchi, bali pande nyingine pia, kama zinajihisi kuwa ni washirika katika Lebanon, zinapaswa zichukue hatua kwa ajili ya kuilinda nchi hiyo…/