Iraq iimesisitiza kuwa haitaruhusu ardhi na anga yake zitumike kutishia usalama wa Iran au wa nchi nyingine yoyote jirani.

Msimamo huo umetangazwa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq Qasim al-Araji wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya hapa mjini Tehran akiwa pamoja na mwenyeji wake Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na kusisitiza: “Iraq haitaruhusu kwa vyovyote vile kutumiwa ardhi yake au anga yake kutishia Iran au nchi yoyote jirani” na akaongezea kwa kusema: “Baghdad inaendelea kufungamana kikamilifu na makubaliano ya usalama iliyotia saini na Tehran”.

Mwezi Agosti, Iraq na Iran zilitia saini mkataba wa maelewano ili kuimarisha uratibu wa usalama kwenye mpaka wao wa pamoja.

Aidha, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Iraq amebainisha kuwa nchi hiyo imewasilisha malalamiko rasmi dhidi ya Israel kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Itakumbukwa kuwa utawala wa kizayuni wa Israel ilifanya mashambulizi ya kivamizi mjini Tehran tarehe 13 Juni, yaliyolenga maeneo ya kijeshi, ya nyuklia, na ya kiraia pamoja na kuwaua kigaidi makamanda wakuu wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia.

Wakati huo, Iraq ilisema, iliwasilisha malalamiko rasmi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani ukiukaji wa anga yake uliofanywa na Israel wakati ilipofanya shambulio dhidi ya Iran.

Al-Araji vilevile amesema, Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani amesisitiza katika mikutano na viongozi kadhaa wa dunia kwamba nchi yake inapinga “kutumiwa kwa namna yoyote anga yake kufanyia mashambulizi dhidi ya Iran”. 

Katika mkutano huo wa pamoja na waandishi wa habari, kwa upande wake Dk Larijani alisema, mazungumzo yake na mshauri wa usalama wa taifa wa Iraq yalihusu masuala kadhaa ya usalama.

“Lakini lengo kuu la mazungumzo yetu lilikuwa kupanua uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili,” alieleza Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na kusisitiza: “ikiwa tunataka uhusiano wetu wa kiuchumi ubaki thabiti, lazima tuimarishe pia ushirikiano wetu wa kiusalama”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *