
Dar es Salaam. Jina lake ni Zuhura Matimbwa, mkazi wa kijiji cha Mtawanya, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Akiwa binti wa wazazi maskini wanaotegemea kilimo cha kujikimu, alihitimu shule ya msingi kwa alama nzuri, akapangiwa shule ya sekondari iliyo karibu na kijiji chake.
Japo awali alipitia changamoto kadhaa na wenzake kama ukosefu wa maabara na walimu wa sayansi kabla mambo kubadilika shuleni hapo kwa jitihada za Serikali, Zuhura hakukata tamaa. Alijitahidi kwa kutumia rasilimali zilizokuwepo shuleni kufanya vizuri.
Baada ya miaka minne ya jitihada, alihitimu kidato cha nne kwa daraja la kwanza na kuendelea hadi kidato cha sita alipopata pia daraja la kwanza. Hatimaye, alisoma chuo kikuu kusomea na kuhitimu shahada ya Uhasibu na Fedha, na sasa ni mkaguzi wa ndani wa katika halmashauri moja hapa nchini.
Kwa juhudi zake, Zuhura anathibitisha kwamba shule za kata zinaweza kuwa daraja la kuingia katika elimu ya juu na hata ajira.
Zuhura ni kielelezo maelfu ya wanafunzi waliopita njia ya shule za kata hadi vyuo, na hatimaye kuingia katika utumishi wa umma, sekta binafsi, au katika ajira binafsi.
Shule hizi pamoja na mengineyo zilianzishwa kuleta fursa ya elimu ya sekondari karibu kwa kila mtoto wa Kitanzania kokote aliko hasa vijijini.
Zimewezesha watoto wa kaya dhaifu kusoma bila kujilaumu kuhusu gharama kubwa za kuhamia mjini.
Takwimu zinaonyesha mwaka 2005 kulikuwa na shule za kata 1,202 lakini hadi 2022 kulikuwa na shule 4,211ambalo ni ongezeko la mara mbili. Hii inaonesha jinsi mpango wa shule za kata ulivyoenea na kuongeza idadi ya shule kwa zaidi ya mara mbili.
Ingawa awali shule za kata zilikuwa na sifa ya kutoa matokeo duni, safari yake imekuwa ikibadilika. Katika mtihani wa kidato cha sita 2021, kati ya shule 100 bora kitaifa, 54 zilikuwa shule za kata. Pia shule za kata zimewahi kuingia kwenye orodha ya shule 10 bora kitaifa katika mtihani wa kidato cha sita. Shule za Kisimiri na Mwandet ni ushahidi tosha kwa namna zilivyoshangaza kwa kuingia kumi bora mwaka 2019.
Matokeo haya yanaonyesha kwamba zikiwezeshwa kwa rasilimali na kuungwa mkono kitaaluma, shule za kata zina uwezo mkubwa wa kuzalisha wahitimu bora.
Kongole Serikali ya awamu ya sita
Serikali ya awamu ya sita imejipanga kupandisha kiwango cha elimu katika shule hizi kwa kuongezea bajeti, kuagiza vifaa vya maabara, kuajiri walimu na kuboresha miundombinu.
Serikali imewekeza zaidi ya Sh 1 trilioni kama bajeti ya elimu kwa kuendelea miradi kwenye sekta ya elimu ( ujenzi wa madrasa,maabara, vitabu, ajira tangu 2021.
Ingawa changamoto kama ukosefu wa walimu, miundombinu duni na bajeti isiyotosha zinakabili, Serikali ya awamu ya sita imeonyesha dhamira ya kuiboresha hali ya elimu, ikipanua uwezo wa shule, kuajiri walimu na kuboresha vifaa.
Mfano mzuri ni ahadi ya hivi karibuni ya mgombea urais Kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ( CCM), Samia Suluhu Hassan, aliyesema ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa atahakikisha anawaajiri walimu 7000 wa masomo ya sayansi na hisabati.
Ni dhahiri shule za kata zinaenda kunufaika na ajira hizi kwa kuwa aghalabu ndizo zenye kilio cha uhaba wa walimu.
Hadithi ya Zuhura ni ushahidi halisi kwamba shule za kata si vikwazo bali vinaweza kuwa nguzo ya mafanikio ya vijana nchini.
Hatuhitaji tena kuzibeza shule hizi zaidi ya kuiunga mkono Serikali pale inapokwama. Ni shule zetu kwani zimekuwa tumaini la watoto wetu.
Shule za sayansi za mikoa
Wakati watangulizi wake walibuni shule za kata ambazo zimekuwa mkombozi kwa mamilioni ya kina Zuhura, Samia naye anataka kuacha urithi wa kutukuka katika historia ya elimu nchini.
Utawala wake ukaja na ubunifu wa kuanzisha shule za sayansi za wasichana za mikoa.
Tayari shule hizi zimeshajengwa katika mikoa 26 zikitumia Sh 116 bilioni gharama za ujenzi wake.Na kama haitoshi Serikali ya awamu ya sita imesema sasa inageukia shule za wavulana.
Natambua huu si mzigo mdogo ambao Serikali ya awamu ya sita imeamua kujitwika.
Kila unapomtazama Samia unaona maono aliyonayo kuhusu elimu ya Taifa letu. Sasa tunaona miundombinu kedekede ikijengwa, hiyo ni tisa lakini kumi ni namna ya kusimamia shule hizi ziwe na Tija.
Changamoto pekee iliyopo sasa ni walimu na vifa hasa vya maabara. Ndicho kilio cha wanafunzi, wazazi na wadau kwa jumla.
Naamini kama siku 100 Samia atafanikiwa kuajiri walimu 7000, miaka mitano ya ngwe yake ya pili, itaacha shule hizi zikiwa na maelfu ya walimu na maabara zilizosheheni vifaa vya kisasa.