Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ambaye pia ni mchambuzi maarufu wa soka hapa nchini, Ally Mayay Tembele, amezipa zaidi ya asilimia 60 timu nne za Tanzania Yanga SC, Simba SC, Azam FC na Singida Black Stars kuvuka hatua inayofuata kwenye mashindano ya kimataifa, licha ya Yanga SC kupoteza mchezo wa kwanza ugenini lakini bado ina nafasi kubwa nyumbani. 

Kwa mujibu wa Mayay, timu za Tanzania zimeanza vyema, ingawa bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho hasa kwa upande wa Yanga SC ambayo imeonekana kupoteza mwelekeo kidogo ukilinganisha na misimu mitatu mfululizo iliyopita.

CA 03

Yanga SC ambayo ni bingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA, ilipoteza ugenini nchini Malawi dhidi ya Silver Strikers ikifungwa bao 1-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Oktoba 18, 2025. Hata hivyo, Mayay anaona bado ina nafasi kubwa kutokana na faida ya kucheza mechi ya marudiano nyumbani.

“Ukiwatazama Yanga SC unaona bado nafasi ipo kwasababu moja ya faida wameanzia ugenini halafu wanakuja kumalizia nyumbani kitu ambacho kinatoa nafasi kwasababu si mara moja Yanga SC wameshawahi kufanya hivyo ugenini lakini wanaporejea katika uwanja wa nyumbani wanarekebisha makosa,” alisema Mayay.

CA 01

Anasema kupungua kwa kiwango cha wachezaji na kushuka kwa ari ya kujituma uwanjani ni mambo yanayohitaji kurekebishwa haraka, lakini historia ya Yanga SC kurejea kwa nguvu inapocheza nyumbani inawapa matumaini makubwa ya kutinga hatua ya makundi.

Kwa upande wa Simba SC, Mayay ameipongeza kwa ushindi wa mabao 3-0 ilioupata dhidi ya Nsingizini Hotspurs FC ugenini nchini Eswatini, akisema matokeo hayo yanaashiria mabadiliko chanya ndani ya kikosi hicho hasa kwenye eneo la washambuliaji ambalo mechi za awali halikuwa katika kiwango kizuri.

CA 04

“Unaona kabisa kuna kitu wamekiongeza hasa eneo la straika, mwalimu amelifanyia kazi na hata jinsi wanavyotoka na mpira nyuma sasa imeanza kurejea. Ni staili yao ya zamani lakini sasa imeboreshwa,” alisema Mayay.

Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Tanzania inawakilishwa na Azam FC na Singida Black Stars, timu zote zimeanza vyema kampeni zao zikiwa ugenini.

Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya KMKM ya Zanzibar, hali inayowapa nafasi kubwa ya kutinga hatua ya makundi hasa ikizingatiwa mechi ya marudiano itafanyika nyumbani. 

GAMO 02

Pia Singida Black Stars ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Flambeau du Centre ya Burundi, matokeo ambayo Mayay ameyataja kuwa yenye thamani kubwa kutokana na faida ya bao la ugenini.

“Hata kama Singida watapata sare ya bila kufungana nyumbani wanavuka hatua ya makundi, ukiangalia usajili wao unaonekana kabisa wamejipanga kwa mashindano ya kimataifa,” amesema Mayay.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *