Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House akiwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, Rais Trump ameeleza kuwa Hamas inafahamu wazi matokeo ya kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano.
Trump ameionya Hamas kwamba iwapo watakwenda kinyume na makubaliano hayo, hatakuwa na budi ila kuliangamiza kundi hilo.
Onyo hilo linaashiria msimamo mkali wa Marekani dhidi ya ukiukaji wowote wa makubaliano huku Marekani ikisisitiza dhamira ya kulinda amani katika eneo la Mashariki ya Kati.
“Tulikuwa na wingu jeusi huko Mashariki ya Kati na sasa, kuna hali tete kidogo na Hamas, japo hali hiyo itashughulikiwa haraka sana na ikiwa Hamas hawataiweka sawa, basi watakuwa wanakiuka makubaliano hayo” ameeleza Trump.
Wasiwasi wa kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha vita
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance ameelekea Israel mara tu baada ya kauli hiyo ya Trump, akiungana na wajumbe wawili wa ngazi ya juu wa Marekani baada ya kushuhudiwa vurugu mwishoni mwa wiki zilizotishia kuvunjika kwa mkataba huo wa kusitisha mapigano.
Trump alikuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mkataba huo yapata wiki mbili zilizopita, ingawa kumekuwa na dalili za mara kwa mara za kuvunjika kwa mkataba wenyewe huku Israel ikiilaumu Hamas kwa kuchelewa kuikabidhi miili ya mateka waliokufa na kwa kuendeleza mashambulizi.
Mpatanishi mkuu wa Hamas Khalil al-Hayya ameliambia shirika la habari la Misri la Al-Qahera News kwamba, kundi hilo limejitolea kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano.
Khalil al-Hayya amesema, “Tunapata changamoto kubwa katika kuitoa miili, lakini tunafanya kila tuwezalo kuitafuta miili hiyo.”
Trump pia amewaonya wanamgambo hao wa Kipalestina dhidi ya kuwanyonga hadharani wapinzani na washirika wanaojaribu kuwakosoa katika wakati ambapo kundi hilo linajaribu kurejesha tena udhibiti wake kwenye Ukanda wa Gaza ulioharibiwa kwa vita.
Kiongozi huyo wa Marekani hata hivyo amesisitiza kwamba jeshi la Marekani halitashiriki moja kwa moja katika kukabiliana na Hamas, akiongeza kwamba nchi kadhaa zimekubali kujiunga na juhudi za kimataifa za kusimamia ujenzi mpya wa Gaza.
Ameeleza kwamba kundi la Hamas limepoteza nguvu, hasa baada ya mshirika wake wa kikanda, Iran kuonyesha dalili za kutojihusisha na mzozo huo baada ya Tehran kushambuliwa na Marekani na Israel mwaka huu.
Wakati hayo yanaendelea, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, imetoa taarifa kuthibitisha kutambuliwa kwa mwili wa mateka aliyerejeshwa jana na Hamas kuwa ni wa Sajenti Meja Tal Chaimi, afisa wa jeshi aliyeuawa Oktoba 7, 2023.
Chaimi, mwenye umri wa miaka 41, ambaye alihudumu kama kamanda wa kikosi cha ulinzi katika eneo la Nir Yitzhak, aliuawa katika siku ya kwanza ya mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7, mwaka 2023. Mwili wake ulichukuliwa na kupelekwa hadi Gaza.
Jukwaa la familia za mateka ambalo ni shirika kuu linalotetea kurejeshwa kwa mateka kutoka Gaza, limesema kwamba Chaimi alionyesha “ujasiri wa kipekee, kwa kupigana kwa saa kadhaa” wakati kulipotokea shambulio la Hamas.
Jana Jumatatu, Israel ilieleza kwamba imepokea mabaki ya mateka mwingine kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na ambayo yalianza kutekelezwa kuanzia tarehe Oktoba.
Hadi sasa Hamas imeirejesha miili 12 ya mateka wa Israel, kati ya miili 28 iliyoahidi kuirejesha kama sehemu ya makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa masharti ya makubaliano hayo, kundi la Hamas lilipaswa kuwaachilia mateka wote wa Israel – walio hai na waliokufa – kufikia tarehe 13 Oktoba.