Hatimaye Nottingham Forest imemtangaza Sean Dyche kuwa kocha mpya wa kikosi hicho, ikiwa ni siku chache baada ya kumfuta kazi Ange Postecoglou.
Mmiliki wa klabu hiyo, Evangelos Marinakis, alichukua uamuzi wa kumfuta kazi Postecoglou dakika 19 tu baada ya kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Chelsea katika uwanja wa nyumbani, City Ground. Hii ilikuwa mechi ya nane mfululizo bila ushindi kwa Postecoglou tangu alipojiunga na Forest mwezi Septemba, 2025.
Forest imekuwa na mwenendo mbaya tangu ilipomfukuza Nuno Espirito Santo mapema msimu huu, baada ya mechi tatu pekee za EPL.
Kabla ya kumtangaza Dyche, kikosi cha Forest kilikuwa chini ya kocha chaguo la tatu klabuni hapo, ambaye ataendelea kufanya kazi chini ya utawala mpya wa benchi la ufundi.
Dyche ambaye amesaini mkataba hadi majira ya joto mwaka 2027, anaungana na Ian Woan na Steve Stone, wote wakiwa ni wachezaji wa zamani wa Forest walioichezea jumla ya mechi zaidi ya 400 kwa pamoja.
Kocha huyo raia wa England, aliwahi kuwa mchezaji wa timu ya vijana ya Forest na anaishi maeneo ya karibu na klabu hiyo, ataanza rasmi kazi kwa kuiongoza timu kwenye mechi ijayo ya Europa League dhidi ya FC Porto, keshokutwa Alhamisi, Oktoba 23, 2025.
Taarifa iliyothibitisha kutangaza kwa Dyche imeeleza: “Kocha mwenye heshima kubwa na uzoefu kwenye Ligi Kuu ya EPL, Dyche ataleta mchanganyiko kamili wa tabia, maarifa ya mbinu, na mafanikio yatakayoakisi, kuiongoza klabu katika sura yake mpya.
“Akiwa ameongoza mechi zaidi ya 330 za EPL, Dyche amekuwa akiunda timu zenye nidhamu ya kiulinzi, uimara, na hatari kwenye mipira ya adhabu, sifa zinazooana kikamilifu kwenye kikosi cha sasa cha Forest.
“Akiwa na uelewa wa maadili na fahari ya klabu na mashabiki wake, Dyche ni chaguo sahihi kwa mafanikio ya msimu huu, kimataifa na kitaifa.”
Dyche alianza kazi ya ukocha Watford kabla ya kuwa na mafanikio makubwa Burnley, akiipandisha daraja kwa bajeti ndogo msimu wa 2013-2014. Ingawa walishuka daraja msimu huo huo, walirejea EPL na kudumu kwa misimu mitano, huku wakiingia Europa League msimu wa 2017-18.
Baadaye aliiongoza Everton kupona kushuka daraja baada ya kampeni mbaya chini ya Frank Lampard, lakini hakuweza kuibadilisha kuwa timu ya zilizomaliza kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa EPL. Alifutwa kazi mwezi Januari 2025.