Dar es Salaam. Kwa miaka yote staa wa BongoFleva, Diamond Platnumz, ameendelea kuthibitisha si msanii wa kawaida bali ni kiongozi anayewabeba na kuwainua wasanii wote walio chini ya lebo yake ya WCB Wasafi.
Ametumia ushawishi na mafanikio yake kuwafungulia njia za kimataifa, kuwatafutia kolabo kubwa na kufanya nao kazi zilizowapa umaarufu zaidi barani Afrika na duniani.
Diamond alianza kusaini wasanii rasmi mwaka 2015, akianza na Harmonize, ambaye kwa sasa ameanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide, iliyoanza kusaini wasanii mwaka 2020 baada ya kuondoka WCB.
Ili kuhakikisha wasanii wake chini ya WCB wanapiga hatua, Diamond amekuwa akitumia juhudi na mbinu mbalimbali za kuwabeba wasanii hao.
Zifuatazo ni njia mbili kuu ambazo amekuwa akizitumia kwa mafanikio makubwa kwa miaka mingi sasa.
Mosi; Kuwatafutia kolabo za kimataifa, sio mara moja wala mbili Diamond amewasaidia wasanii wake kupata kolabo na mastaa wa kimataifa ambao yeye mwenyewe amewahi kufanya nao kazi hapo awali. Hii imekuwa moja ya njia muhimu zaidi alizotumia kuwapa nafasi kubwa zaidi ya kujulikana.

Mfano ni mwaka 2017, ambapo baada ya Patoranking kutoka Nigeria kumshirikisha Diamond kwenye wimbo ‘Love You Die’, Chibu alitumia nafasi hiyo kumtafutia Rich Mavoko kolabo na Patoranking kwenye wimbo ‘Rudi’ uliotoka Oktoba mwaka huo.
Bila shaka, Rudi ndiyo kazi kubwa zaidi ya kimataifa aliyowahi kufanya Rich Mavoko akiwa WCB. Video ya wimbo huo ilifanyika Uingereza na kufanya vizuri kwenye chati mbalimbali za redio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Baada ya mafanikio ya Yope Remix (Septemba 2019) iliyomshirikisha Innoss’B kutoka DR Congo, Diamond aliufungua mlango kwa Zuchu na Rayvanny (ambaye sasa ameondoka WCB).
Rayvanny alimshirikisha Innoss’B katika wimbo ‘Makelebe’ uliopo kwenye albamu yake ya kwanza, Sound From Africa (2021).
Miaka miwili baadaye, yaani Juni 2023, Zuchu naye akafanya kolabo na Innoss’B kwenye ngoma yake ‘Nani Remix’ uliopata mapokezi mazuri. Bila ushawishi wa Diamond, kufanikisha kolabo hizo kungekuwa kugumu zaidi kwa wasanii hao.
Katika EP yake, First of All (FOA) iliyotoka Machi 2022, Diamond alimshirikisha Costa Titch wa Afrika Kusini kwenye wimbo ‘Fresh’ ambao pia uliwashirikisha Focalistic na Papi Cooper.

Miezi michache baadaye, Costa Titch kabla ya kifo chake Machi 2023 alisikika tena kwenye wimbo wa Mbosso, ‘Shetani’, uliomo kwenye EP yake ya kwanza, Khan (2022).
Aidha, moja ya ngoma maarufu kwenye albamu ya tatu ya Diamond, A Boy From Tandale (2018), ni ‘Hallelujah’ aliyofanya na kundi la Morgan Heritage kutokea Jamaica. Baadaye, Harmonize naye akaja kufanya kazi na kundi hilo kwenye albamu yake ya kwanza, Afro East (2020), ingawa ilikuwa baada ya kuondoka WCB Wasafi.
Pili; Kufanya kolabo nyingi nao ni desturi ya Diamond kushirikiana na kila msanii mpya anayemsaini WCB Wasafi, hasa muda mfupi baada ya kuwatambulisha rasmi. Kolabo hizi zimekuwa na mafanikio makubwa, mara nyingi zikibaki kuwa kazi zao bora zaidi hadi leo.
Miongoni mwa waliopata fursa hiyo ni Harmonize, ambaye alimshirikisha Diamond kwenye nyimbo mbili, Bado (2016) na Kwangwaru (2018) wimbo uliotikisa sana Afrika Mashariki. Hadi sasa, Kwangwaru ndio video pekee ya Harmonize iliyofanya vizuri zaidi YouTube ikitazamwa mara milioni 132.
Rayvanny ndiye msanii aliyenufaika zaidi na ushirikiano na Diamond na wawili hao wameshirikiana kwenye nyimbo zaidi ya 10 ambazo ni Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022), Yaya (2023) na Nesa Nesa (2024).
Kwa upande wa Mbosso akiwa bado WCB Wasafi, alishirikiana na Diamond katika nyimbo kama Jibebe (2018), Karibu (2021), Oka (2022), Yataniua (2022) na Baikoko (2021) ambao ndio wimbo wa Mbosso uliofanya vizuri sana YouTube ukiwa umetazamwa mara milioni 67.
Tukija kwa Zuchu, hadi sasa huyu ndiye msanii pekee wa kike Bongo aliyepewa nafasi zaidi na Diamond wakifanya kolabo sita ambazo ni Cheche (2020), Litawachoma (2020), Mtasubiri (2022), Raha (2024), Walewale (2024) na Inama (2025).
Kolabo zao mbili za mwanzo, zilipokelewa kwa shangwe kubwa na zikamtambulisha zaidi Zuchu kwenye ramani ya muziki wa Afrika Mashariki, na sasa muziki wake ukiwa amesambaa hata nje ya kanda hiyo.
Kwa upande wake Rich Mavoko, wimbo wake wa pili chini ya WCB Wasafi, Kokoro (2016), alimshirikisha Diamond. Ulifanya vizuri sana ingawa video yake iliondolewa YouTube mara baada ya mgogoro uliosababisha kuondoka kwake kwenye lebo hiyo.
Lava Lava naye ambaye ameondoka WCB Wasafi mapema mwaka huu ikiwa ni baada ya miaka saba ya kufanya kazi pamoja, alishirikiana na Diamond katika ngoma kama Jibebe (2018), Far Away (2021), Bado Sana (2021), Tuna Kikao (2023) na Kibango (2024).

Hadi sasa, Queen Darleen ambaye aliondoka kimya kimya, ndiye msanii pekee wa WCB ambaye hajawahi kufanya kolabo ya moja kwa moja na Diamond, ingawa wote walishiriki kwenye nyimbo za pamoja za lebo hiyo kama Zilipendwa (2017) na Quarantine (2020).
Naye D Voice, mwanamuziki wa mwisho kutambulishwa WCB Wasafi, yeye amefanya kolabo moja tu na Diamond iitwayo ‘Kama Wengine’ kutoka katika albamu yake, Swahili Kid (2023). Hivyo kwa ujumla, Diamond amefanya kolabo 32 na wasanii wake wake nane.