
Dodoma. Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma imeikubali rufaa iliyokatwa na Clinton Damas, maarufu Nyundo na wenzake watatu waliotiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti kwa kundi, ikieleza kosa hilo halipo katika sheria.
Hata hivyo, mahakama hiyo imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela walichohukumiwa washtakiwa hao kwa kosa la kubaka kwa kundi, hivyo wataendelea kutumikia adhabu hiyo, ambayo haina mbadala.
Mbali ya Nyundo, aliyekuwa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), warufani wengine ni Amin Lema maarufu Kindamba, Nickson Jackson ‘Machuche’ na aliyekuwa askari Magereza, Praygod Mushi.
Nyundo na wenzake walitiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma Septemba 30, 2024, kwa kosa la kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, wakahukumiwa kifungo cha maisha jela na walitakiwa kumlipa mwathirika Sh1 milioni kila mmoja kwa kumsababishia maumivu.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne, Oktoba 21, 2025 na Jaji wa Mahakama Kuu, Amir Mruma. Amesema hakuna kosa la kulawiti kwa kundi, bali adhabu hutolewa kwa mtu mmojammoja aliyetenda kosa hilo.
Ameeleza kwa kosa la kubaka kwa kundi, sheria inaeleza adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani na hakuna mbadala wa adhabu hiyo, hivyo warufani wataendelea kutumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kubaka kwa kundi.
Jaji Mruma amesema sheria haina mbadala wa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kubaka kwa kundi, hivyo ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba, haitoi nafasi kwa washtakiwa kujifunza na kujirekebisha.
Jaji Mruma amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 107 A (1) inaeleza mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa Mahakama, lakini sheria ya mtu atakayepatikana na hatia ya kubaka kwa kundi inaonekana kuwa juu ya Katiba kwani haiipi mamlaka Mahakama kuamua kinyume cha adhabu ya kifugo cha maisha gerezani.
“Kwa hiyo kwenye kosa hili la kubaka kwa kundi sheria imeifunga mikono mahakama kwa sababu hakuna adhabu mbadala ya kifungo cha maisha, hii inaonyesha kuwa sheria hiyo ipo juu ya Katiba ambayo inatamka kuwa mahakama ndiyo yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki. Sheria hii inapaswa kuangaliwa upya,” amesema.
Jaji Mruma amesema kwenye makosa ya kubaka sheria imeeleza wazi kuwa mtu akimwingilia kimwili kwa nguvu mtu mwingine ni kosa na lina adhabu yake na kikundi cha watu kikimwingilia kimwili mtu mwingine bila ridhaa yake ni kosa na adhabu yake ni kifungo cha maisha gerezani.
“Hii adhabu haitoi nafasi kwa washtakiwa kujifunza kwa sababu adhabu zote zinazotolewa huwa ni kwa ajili ya kuwafanya waliotenda kosa hilo kujutia na kujirekebisha, lakini adhabu ya kifungo cha maisha na adhabu ya kifo haitoi nafasi ya washtakiwa kujifunza na kujirekebisha, ukichukulia umri wa hawa watoto bado ni wadogo na walikuwa hawajui kosa wanalolitenda kama lingewafikisha hapa,” amesema.
Amesema vijana hao wenye umri kati ya miaka 23 hadi 27 ni wadogo na wakati wakitenda kosa hilo akili zao bado zilikuwa hazijapevuka, lakini wanalazimika kutumikia adhabu hiyo kwa sababu hakuna nyingine iliyotolewa na sheria ya kubaka kwa kundi.
Amesema hata sababu ya kutenda kosa hilo haikuwa imedhamiriwa kwa sababu mwathirika wa tukio hilo alikubaliana na mtu mmoja ambaye walifanya naye mapenzi kwa hiari, lakini vijana hao walivamia chumba hicho na kumlazimisha binti huyo kufanya naye mapenzi kwa nguvu bila kujua kitendo hicho kingewasababishia matatizo makubwa.
Jaji Mruma amesema ipo haja ya kuzipitia sheria upya ili ziendane na wakati, ikiwamo sheria ya kulawiti kwa kundi na ile ya kubaka kwa kundi ili kutoa adhabu mbadala kwa washtakiwa kuliko ilivyo sasa ambapo mahakama haina mamlaka dhidi ya sheria hizo.
Akizungumzia ushahidi uliowatia hatiani washtakiwa hao, amesema ni uliotolewa na shahidi wa tatu ambaye ni mwathirika wa tukio hilo na ushahidi wa video walizojirekodi wakati wakitenda tukio hilo zilizopokewa mahakamani, ambazo ziliwaonyesha kila mmoja akitenda kosa la kubaka na kulawiti.
Amesema mahakama imetupilia mbali rufaa ya kupinga adhabu ya kubaka kwa kundi kwa sababu video zilizoletwa mahakamani kama ushahidi ziliwaonyesha washtakiwa wote wakishiriki kufanya uhalifu huo na hakuna hata mmoja aliyepinga mahakamani kuwa si yeye aliyekuwa akionekana kwenye video hizo.
“Kama wangekana kuwa wale wanaoonekana kwenye video si wao, uchunguzi wa kina ungefanyika lakini hakuna hata mmoja aliyekataa kuwa si yeye anayeonekana mle kwenye video, wangesema siyo wao labda ni AI (akili unde) zingechunguzwa lakini kwa sababu hawakukataa hapakuwa na sababu za kuchunguza video hizo,” amesema.
Jaji amesema baada ya kupitia hoja zilizotolewa na warufani na wajibu rufaa, huo ndiyo uamuzi wa mahakama na kama kuna mtu hajaridhika anaweza kukata rufaa.
Katika rufaa hiyo, warufani waliwakilishwa na mawakili Godfrey Wasonga, Robert Owino na Meshack Ngamando, huku wajibu rufaa (Jamhuri) ikiwakilishwa na mawakili Lucy Uisso, Ahmed Mtenga na Aziza Mhina.
Warufani walikuwa na hoja 33 za rufaa walizoziweka kwenye mafungu tisa. Miongoni mwa sababu za rufaa ni kukosewa kwa hati ya mashtaka, kutothibitisha kosa bila kuacha shaka na kushindwa kuwakamata watuhumiwa wengine wawili.
Jaji Mruma amesema ni hoja moja pekee ya kosa la kulawiti kwa kundi ndiyo iliyokubaliwa na kuwaondolea hatia wakata rufaa, kwani sheria ya kulawiti kwa kundi iliyowatia hatiani haipo nchini.
Amesema hoja nyingine zilizowasilishwa mahakamani hapo hazikuwa na nguvu kwa sababu hazikuathiri upatikanaji wa haki na hakuna hata mmoja aliyelalamika kukosa haki kutokana na kuwepo kwa hoja hizo, ikiwamo kukosewa kwa hati ya mashtaka, kukosewa kwa jina la mahakama iliyotoa hukumu na ile iliyoandikwa kwenye hati ya mashtaka na gwaride la utambuzi.
Kuhusu maelezo ya onyo, Mahakama imesema mkata rufaa wa kwanza (Nyundo) alitoa maelezo ya onyo na kukiri kubaka kwa kundi na kulawiti kwa kundi bila kuteswa, kutishwa wala kudanganywa, hivyo inaonyesha ni kwa namna gani alitenda kosa hilo.
Nje ya mahakama
Wakili Mkuu wa Serikali, Lucy Uisso amesema wameona upungufu uliopo kwenye sheria ya makosa ya kubaka kwa kundi na yale ya kulawiti na kwamba, ipo haja ya kufanyia marekebisho sheria hizo ili ziweze kwenda na wakati.
Amesema wakati wa kutunga sheria ya kulawiti haikufikiriwa kuwa kungekuwa na kulawiti kwa kundi, ndiyo maana sheria haijatamka adhabu za kulawiti kwa kundi na adhabu mbadala ya kubaka kwa kundi, ambayo imeonekana inapingana na Katiba ya nchi.
Wakili Godfrey Wasonga, amesema bado kuna nafasi ya kukata rufaa ambayo wataitumia ili kuhakikisha wateja wao wanapata haki.