
Dar es Salaam. Msanii wa Hip Hop, Abdullah Jamal Mnete ‘Zaiid’ amesema licha ya baadhi ya nyimbo zake kuwa na majina yanayowaelezea wanawake, haimaanishi maudhui yake yanawalenga wanawake moja kwa moja, bali inafikisha ujumbe kwa mashabiki wake wote kwa njia ya fasihi.
Zaiid amesema uandishi ni sanaa na ubunifu, hivyo nyimbo zake alizozitoa zinazoelezea wanawake baadhi ni Pisi Kali alioshirikiana na P-Mawenge, Tafuta Bwana alioimba na Belle 9, Demu Noma ft P Mawenge na Wowowo, zipo zinazowalenga wanawake moja kwa moja na zile zinazowalenga wanaume.
“Mfano wimbo wa Pisi Kali ndani yake unaongelea wanaume ambao wanafeli maisha, ujumbe ninaowafikishia ni wafanye kazi kwa bidii waache kuwa kama pisi kali, Tafuta Bwana unawakumbusha watu kufunga ndoa na pia kumrudia Mungu,” amesema na kuongeza;
“Ndiyo maana naitwa Zaiid nikiwa na maana ya Zaiid yao, nikimaanisha nyimbo zangu zipo kuwafikia watu fulani ili kuhakikisha naelimisha jamii na kuburudisha.”
Mbali na hilo, alizungumzia ukimya wake wa kutoachia nyimbo kwa muda mrefu akisema alikuwa anaziandaa nyingine, hivyo anatarajia kuachia wimbo mmoja mmoja kila wiki.
“Nina nyimbo zinafika takribani 300, nitakuwa naachia kila wiki wimbo mmoja, nyingi zitakuwa na majina ya kike, ila ujumbe wake unalenga kitu kingine kabisa, hivyo mashabiki wangu wajiandae kwa kuusikiliza muziki mzuri,” amesema staa huyo wa Tafuta Bwana na Wowowo.