
KIUNGO wa zamami wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Jonas Mkude amesikitishwa na kifo cha mchezaji wa zamani wa timu hizo, Alphonce Modest aliyefariki dubnia jioni ya Oktoba 21, 2025.
Mkude ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kumpa msaada Modest aliyewahi pia kuichezea Mtibwa Sugar.
Katika mahojiano na Mwanaspoti na Modest wakati wa uhai wake yaliyofanyika Novemba, 2024 Modest aliwahi kuelezea wema aliofanyiwa na Mkude, kwamba alimkutaka katika hali mbaya na akampatia pesa za kumsaidia kujikimu.
Katikati ya mahojiano hayo mwandishi alipimgia simu Mkude akiwa na Modest ambapo walisalimiana na kupeana pole.
Baada ya kupta taarifa za msiba, Mkude amesema:” Nakosa neno la kusema, lakini nimejifunza kumjali mtu akiwa katika shida ili shukrani yake aitoe kwa kinywa chake akiwa hai.
Ameongeza: “Alponve alikuwa lejendari, alistahili heshima, upendo kutokana na jasho lake alilovuja uwanjani. Pia nikushukuru mwandishi ulipofika (kwa Modest) ukapiga simu nikazungumza naye. Kumbukumbu ya maongezi yetu itasalia kwangu.
“Naishiwa maneno Mungu ampumzishe kwa amani, kwani ana sababu ya kila jambo, sisi ni wanadamu tunapita.”
Hayati Modest aliwahi kumtaja Mkude kuwa ni miongoni mwa vipaji vikubwa nchini.
Siku tatu kabla ya umauti Modest alizungumza na Mwanaspoti namna alivyokuwa anajisikia.
“Nimechoka sana mwandishi, nasubiri muujiza wa Mungu kunichukua ili ndugu zangu wapumzike, maana nimeugua kwa muda mrefu. Kwa sasa hakuna ninachokitamani tena.”
MASTAA WENGINE WALIOMLILIA
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella amesema: “Inaumiza sana, lakini muache akapumzike kwa amani mchango wake katika taifa utakumbukwa.”
Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba, Steven Mapunda ‘Garincha’ amesema: “Kwa wachezaji waliomuona akicheza hadi akaazimwa Simba kwenda Yanga kwa ajili ya michuano ya kimataifa wanajua. Kazi yake Mungu ampumzishe kwa amani.”