KOCHA wa KMC, Marcio Maximo amekiri vitatu mfululizo ambavyo wamekumbana navyo kwenye ligi, vinamnyima usingizi na bado anatafuta mchanganyiko sahihi wa wachezaji watakaorudisha chama hilo katika njia sahihi ya ushindi.
KMC ilianza msimu kwa matumaini makubwa baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Dodoma Jiji, hata hivyo, hali iligeuka ghafla baada ya vijana hao wa Manispaa ya Kinondoni kupoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya Singida Black Stars, Tanzania Prisons na Mbeya City matokeo yaliyowaacha katika nafasi ya 14 kati ya timu 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kocha Maximo amesema hana hofu, bali anahisi msukumo wa kufanya marekebisho ya haraka.

“Tumeanza vizuri, lakini tumejikuta tukipoteza mwelekeo. Hii ni ligi ndefu na bado tuna nafasi ya kurekebisha makosa yetu.”
Mtaalamu huyo kutoka Brazil amesema changamoto kubwa aliyokutana nayo ni wachezaji kushindwa kuwa makini muda wote wa mchezo, hali iliyowagharimu katika mechi walizopoteza.
“Tunatengeneza nafasi, tunashindwa kuzitumia, halafu tukafanya makosa, hivyo tuna kazi ya kufanya kubadili mambo.”
Maximo amesema amekuwa akitumia muda mwingi mazoezini kurekebisha safu ya ulinzi na namna ya kuunganisha viungo na washambuliaji, akiamini kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi kutaimarisha kikosi chake.

Kocha huyo pia amewataka mashabiki wa KMC kuwa wavumilivu huku akiahidi mabadiliko anayoyafanya yataanza kuonekana hivi karibuni.
“Najua mashabiki wanataka matokeo ya haraka, lakini wachezaji wanahitaji muda wa kujenga uelewano. Tutarejea tukiwa imara zaidi,” amesema.

Kwa mujibu wa ratiba, KMC inakabiliwa na michezo miwili migumu mfululizo ugenini dhidi ya Fountain Gate na mabingwa watetezi Yanga.