Taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na afisa mmoja wa serikali ya Washington ambaye hakutaka kutajwa jina lake, imesema kuwa mkutano uliokuwa ukitarajiwa kufanyika kati ya marais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin huko Budapest nchini Hungary umesimamishwa kwa muda baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kufanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov na kushindwa kuafikiana kuhusu suala nyeti la kusitisha mapigano katika  vita vya Ukraine.

Trump amethibitisha taarifa hiyo akisema haitaji kuwa na mkutano usio na tija wala kupoteza muda akiongeza pia  kwamba kwa sasa wanasubiri kuona kitakachofuata akisisitiza kuwa pande zote zinaendelea kupata hasara kubwa kwa kuwapoteza wanajeshi wao na ndio maana amani inahitajika. Lakini upande wa Moscow wamesema maandalizi ya mkutano huo kati ya Trump na Putin yanaendelea na kwamba kunahitajika kukubaliana katika mambo kadhaa muhimu.

Ulaya yaunga mkono juhudi za Trump

Viongozi wa Ulaya wakiwemo wale kutoka Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya wakishirikiana na Ukraine walitoa taarifa ya pamoja siku ya Jumanne wakitaja kuunga mkono mwito wa Rais wa Marekani Donald Trump wa usitishwaji wa mapigano kati ya Urusi na Ukraine. Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa viongozi hao wa Ulaya akiwemo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky watakutana Ijumaa wiki hii mjini London katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kujadili namna ya kuendelea kuiunga mkono Kiev.

Denmark I Viongozi wa Ulaya walipokuwa kwenye mkutano
Viongozi wa Ulaya walipokuwa kwenye mkutano nchini DenmarkPicha: Sebastian Elias Uth/Ritzau Scanpix/IMAGO

Licha ya viongozi wa Ulaya kuunga mkono juhudi za amani zinazosimamiwa na rais wa Marekani, taarifa hii ya kusitishwa kwa mkutano huo kati ya Trump na Putin imepokelewa kama ahueni kwa viongozi hao wa Ulaya ambao wamekuwa wakimshutumu Putin kujaribu kujipatia muda zaidi kupitia michakato hii ya kidiplomasia huku akijiimarisha katika uwanja wa vita.

Viongozi wa Ulaya akiwemo Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na hata Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz walisema waziwazi kuwa wanapinga wa mchakato wowote wa amani utakaoilazimisha Ukraine kusalimisha maeneo ya ardhi yake yaliyonyakuliwa na vikosi vya Urusi, kama ilivyopendekezwa mara kwa mara na Trump.

Aidha viongozi hao wa Ulaya wanajaribu kufanikisha mpango wa kutumia mabilioni ya dola ya mali za Urusi zilizozuiwa ili kuisaidia Ukraine kuendelea kukabiliana na Urusi, licha ya mashaka kuhusu uhalali wa hatua hiyo na matokeo yanayoweza kushuhudiwa. Rais Zelensky amesema Urusi bado ina nia ya kutwaa eneo zima la nchi ya Ukraine akisisitiza kuwa maelfu ya wanajeshi watahitajika ili kutoa hakikisho la usalama baada ya vita.

Katika hatua nyingine, Trump anatarajiwa siku ya Jumatano kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya  NATO  Mark Rutte. Ingawa haijawekwa wazi watakachojadili, ifahamike tu kuwa NATO ndio imekuwa na jukumu la kuwasilisha nchini Ukraine silaha zote zinazotolewa na Marekani na washirika wake wa Ulaya.

//AP, DPA, RTR, AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *