
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa, watu zaidi ya milioni moja wamerejea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, katika kipindi cha miezi 10 iliyopita licha ya kukosekana usalama wa kutosha katika mji huo kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Operesheni wa IOM, Ugochi Daniels ameeleza katika taarifa yake: “kiwango cha watu kurejea Khartoum ni ishara ya uhimilivu wa watu, lakini pia ni indhari”.
“Nilikutana na watu wanaorejea katika jiji ambalo bado lina athari za vita – nyumba zimeharibiwa na huduma za msingi hazifanyi kazi ipasavyo. Uamuzi wao wa kuanza upya ni wa kushangaza, licha ya kuwa maisha bado ni hatarishi sana”, ameeleza afisa huyo wa IOM.
IOM imeonya kuwa wengi wa waliorejea wanaishi katika nyumba zilizoharibika au makazi yenye msongamano mkubwa, huku wakiwa na upungufu mkubwa wa maji safi, huduma za afya, au ulinzi. Magonjwa kama kipindupindu na malaria yanaendelea kuenea.
Khartoum ingali ni makazi ya watu zaidi ya milioni 3.7 waliopoteza makazi yao, na wale waliorejea hadi sasa ni asilimia 26 tu ya jumla hiyo.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linakadiria kuwa watu milioni 2.7 zaidi wanaweza kurejea baadaye, kutegemea na hali ya usalama na misaada ya kibinadamu.
Hadi sasa, watu milioni 2.6 wameweza kurejea katika maeneo yao ya awali tangu mwishoni mwa 2024, wakiwemo zaidi ya nusu milioni waliokuwa uhamishoni nje ya nchi, hususan kutoka Misri, Sudan Kusini, na Libya.
Kwa upande wa Khartoum, taasisi ya Sudan Return Monitoring Snapshot imesema, ilirekodi kurejea kwa watu hao kati ya Novemba 2024 na Septemba 2025, huku familia zikihama kutoka maeneo mengine ya nchi na hata kutoka mataifa ya nje.
Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi Machi, jeshi la Sudan lilidai kuwa limewafurusha wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF kutoka Khartoum, takriban miaka miwili baada ya kupoteza udhibiti wa mji huo kwa kundi hilo la wanamgambo.
Mapigano kati ya jeshi na RSF yalianza mwezi Aprili 2023, na yamesababisha vifo vya maelfu ya watu…/