Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu Yemen imefanikiwa kuwa nchi ya kwanza kati ya nchi zote za Kiarabu katika uzalishaji wa silaha na zana za kijeshi. Uzalishaji wa kombora katika nchi yetu uko kwenye njia inayozidi kustawi na tuna mafanikio makubwa katika uzalishaji wa droni na ndege zisizo na rubani.

Sayyid Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi amesema hayo katika hotuba yake ya jana Jumanne kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Meja Jenerali Mohammed Abdul Karim al-Ghammari, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Yemen.

Akizungumzia umati mkubwa wa watu ulioshiriki kwenye maziko ya kamanda huyo mwanamapambano juzi Jumatatu, Sayyid al-Houthi amesma: “Jana (akikusudia juzi Jumatatu), taifa letu pendwa, lilijitokeza kwa wingi mno kwenye maziko ya Mkuu wa Majeshi, shahidi wetu mtukufu, Mohammed Abdul Karim al-Ghammari na umati huo mkubwa wa watu unaonesha jinsi wananchi wetu walivyo na msimamo thabiti usioyumba.

Akigusia msimamo wa Yemen wa kuendelea kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza huko Palestina, Kiongozi wa Ansarullah Yemen amesema: “Shahidi Al-Ghammari na mashahidi wengine katika vita vya “Ushindi Ulioahidiwa” na “Jihad Tukufu”  ni nembo kuu za uaminifu na nafasi adhimu ya taifa letu pendwa. Taifa letu la Yemen limenyanyua juu bendera ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwasaidia watu wa Palestina na kushikamana na masuala makubwa ya kitaifa dhidi ya madhalimu wakuu wa zama hizi yaani Marekani na Israel.

Aidha amesema: “Vita vikali sana vilivyoendelea kwa muda wa miaka miwili iliyopita vimefichua mambo mengi na vimeonesha misimamo ya watu huru walioitikia mwito wa Mwenyezi Mungu na kuongozwa na imani, motisha wa kiutu na kimaadili ambao walichukua msimamo sahihi wa kuwaunga mkono Wapalestina na wanamapambano wake wapendwa. Vita hivyo vimewafichua pia wale waliokwenda kinyume, ambao walijitokeza waziwazi kumsaidia Israel na mwisho wamefedheheka na kuaibika.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *