
Chanzo cha picha, John Heche
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, John Heche amekamatwa asubuhi hii akiwa nje ya Mahakama Kuu kuhudhuria kesi inayomkabili yeye na viongozi wengine wa chama, pamoja na kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amedai kuwa Heche amekamatwa na Jeshi la Polisi asubuhi ya leo alipokuwa akiwasili mahakamani.
”Tumekwishaelekeza mawakili wetu, waelekee moja kwa moja polisi kwenda kufuatilia suala hili.” alisema Mnyika.
Jeshi la polisi halijasema sababu za kukamatwa kwake.
Heche alikamatwa mwishoni mwa juma lililopita mkoani Mara kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya huko Isibania One Stop Border alipokuwa anataka kuingia Kenya.
Kwa mujibu wa CHADEMA, Heche alikuwa akiingia nchini Kenya kukiwakilisha chama kwenye shughuli za mazishi ya mwanasiasa nguli wa Kenya,Raila Amolo Odinga.
Pamoja na kumuweka kizuizini taarifa ya chama hicho ilisema kuwa, Mamlaka ya Uhamiaji Tanzania ilimnyang’anya hati yake ya kusafiria.
Idara ya Uhamiaji ilisema kwenye taarifa yake kuwa Heche aliondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za Uhamiaji.
Ilitoa wito kwa Watanzania na wageni wanaotoka na kuingia Tanzania kufuata utaratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wawatu nchini ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
John Mnyika amesema madai ya Idara ya Uhamiaji kuwa Heche alivuka mpaka kuingia Kenya kinyume cha utaratibu si ya kweli na kuhusisha madai hayo na kitendo cha kumkamata hii leo.
”Kama kukamatwa kwake kunahusiana na taarifa hiyo ni jambo la kusikitisha sana polisi kutumia taarifa isiyo ya kweli ya uhamiaji kumkamata. Mimi ninafahamu kulikuwa tayari kuna njama huko nyuma kutafuta namna ya kutukamata viongozi kabla ya tarehe 29 Oktoba hivyo vitatumika visingizio mbalimbali”. Alisema Mnyika.