
Kufuatia kifo cha staa wa zamani wa Simba na Yanga, Alphonce Modest kilichotokea jana Jumanne Oktoba 21, 2025 akiwa nyumbani kwao Kigoma, wadau mbalimbali wa soka wamemlilia zikiwemo klabu alizowahi kuzitumikia.
Modest ambaye enzi za uhai wake alikuwa beki wa kushoto, mbali na Simba, Yanga, pia amecheza Pamba, Mtibwa Sugar na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetuma salamu zake za rambirambi kufuatia msiba huo kwa kusema: “Pumzika kwa amani Alphonce Modest.”
Kwa upande wa uongozi wa Mtibwa Sugar, umesema: “Tunasikitika kuwatangazia kifo cha aliyekuwa mchezaji wetu Alphonce Modest Pambamotosapi kilichotokea jioni ya leo (jana Oktoba 21, 2025).
“Modest aliitumikia Mtibwa Sugar kwa mafanikio msimu wa 2001-2006 alipoamua kutundika daluga. Familia ya mpira imempoteza mchezaji nguli ambaye aliichezea timu ya taifa kwa zaidi ya miaka 10.
“Tunaungana na familia, marafiki na wote walioguswa katika kuomboleza msiba huu mzito. Pumzika kwa amani Modest.”
Uongozi wa Klabu ya Simba, nao umesema: “Uongozi wa klabu ya Simba umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa aliyekuwa nyota wetu wa zamani Alphonce Modest kilichotokea jana nyumbani kwao mkoani Kigoma. Modest ambaye alikuwa mlinzi wa kushoto mahiri katika miaka ya 90.
“Simba inaungana na Wanamichezo wote kuomboleza msiba huu mzito na tunawaombea kwa Mungu wafiwa kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu.”
Enzi za uhai wake wakati Modest anasumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, Mwanaspoti liliwahi kumfanyia mahojiano kwa kwenda kumtembelea nyumbani kwao Kigoma ambapo lilishuhudia mateso yake, alikuwa hawezi kugeuka, kichwa chake kikiwa kimetazama juu hata akipita mdudu hakuweza kujitoa bila msaada wa ndugu zake.