Wafanyakazi wa Ukraine wanafanya kazi kwenye tovuti ya shambulio la anga kwenye jengo la kibinafsi huko Kharkiv, kaskazini-mashariki mwa Ukraine, Oktoba 21.

Chanzo cha picha, EPA

    • Author, Anthony Zurcher
    • Nafasi, North America correspondent

Taarifa kwamba kungekuwa na mkutano wa kilele kati ya viongozi wa Marekani na Urusi zimeonekana kuwa za kupotosha.

Ni siku chache tu baada ya Donald Trump kutangaza kuwa alipanga kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, huko Budapest “katika kipindi cha wiki mbili au zaidi”, sasa mkutano huo umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

Hata kikao cha maandalizi kilichopaswa kufanyika kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili kimefutwa.

“Sipendi kushiriki mkutano usio na tija,” Trump aliwaambia waandishi wa habari Jumanne jioni akiwa Ikulu ya White House. “Sitaki kupoteza muda, kwa hiyo tutaona ni nini kitatokea.”

Pia unaweza kusoma:

Mkutano huu wa kuahirishwa na kurudishwa umekuwa sehemu ya jitihada zisizo na mwelekeo wa Trump kutafuta suluhu ya vita vya Ukraine, suala ambalo limepata uzito mpya kwake baada ya kusaidia kufanikisha makubaliano ya usitishaji vita na kuachiliwa kwa mateka huko Gaza.

Akiwa nchini Misri wiki iliyopita kusherehekea mafanikio hayo, Trump alimgeukia mpatanishi wake mkuu wa kidiplomasia, Steve Witkoff, na kutoa agizo jipya:

“Lazima tumalize suala la Urusi,” alisema.

Lakini hali si sawa na Gaza…

Hata hivyo, mazingira yaliyowezesha mafanikio ya Gaza kwa Witkoff na timu yake huenda yakawa magumu kurudiwa katika mzozo wa Ukraine, ambao umeendelea kwa karibu miaka minne sasa.

Kiwango chini ya wastani

Kwa mujibu wa Witkoff, kilichowezesha kufikiwa kwa makubaliano Gaza ilikuwa hatua ya Israel kuwashambulia wapatanishi wa Hamas waliokuwa wakifanya mazungumzo huko Qatar hatua iliyowaudhi washirika wa Kiarabu wa Marekani, lakini iliyompa Trump ushawishi wa kumlazimisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kufanya makubaliano.

Trump alinufaika na historia yake ya kuiunga mkono Israel tangu kipindi chake cha kwanza madarakani, ikiwa ni pamoja na kuhamishia ubalozi wa Marekani Jerusalem, kuhalalisha makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi, na kuunga mkono mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran.

Kwa hakika, umaarufu wa Trump miongoni mwa Waisraeli unazidi ule wa Netanyahu jambo lililompa ushawishi wa kipekee.

Pia, kutokana na uhusiano wake wa karibu wa kisiasa na kiuchumi na baadhi ya mataifa muhimu ya Kiarabu, Trump alikuwa na nguvu kubwa ya kidiplomasia ya kusukuma makubaliano.

Lakini hali ni tofauti kabisa katika vita vya Ukraine.

Trump hana ushawishi mkubwa. Katika miezi tisa iliyopita, amekuwa akibadilika kati ya kumshinikiza Putin na kisha Zelensky bila mafanikio ya maana.

Trump ametishia kuiwekea Urusi vikwazo vipya kwenye sekta ya nishati, na pia ameahidi kuipatia Ukraine silaha za masafa marefu.

Lakini pia ametambua kuwa hatua hizo zinaweza kuvuruga uchumi wa dunia na kuongeza hatari ya vita kupanuka.

Wakati huo huo, Trump amekuwa akimkosoa Zelensky hadharani, akasitisha kwa muda ushirikiano wa kijasusi, na pia misaada ya kijeshi kabla ya kubadili msimamo baada ya mashinikizo kutoka kwa washirika wa Ulaya waliotahadharisha kuwa kusambaratika kwa Ukraine kunaweza kuiyumbisha Ulaya nzima.

Ingawa Trump hupenda kusisitiza uwezo wake wa kufanya mikutano ya ana kwa ana na kufanikisha makubaliano, vikao vyake na Putin pamoja na Zelensky havijaleta mafanikio yoyote ya kupunguza vita.

Trump na Putin wakiwa wamekaa karibu wakati wa mkutano wa kilele kuhusu Ukraine mwezi Agosti.

Chanzo cha picha, Getty Images

Putin anacheza karata ya Trump

Huenda Putin anatumia tamaa ya Trump ya kufanikisha makubaliano kama njia ya kumshawishi.

Mwezi Julai, Putin alikubali kufanyika kwa mkutano nchini Alaska wakati ambapo Trump alikuwa karibu kuidhinisha kifurushi cha vikwazo kutoka kwa wajumbe wa seneti mrengo wa kushoto.

Baada ya tangazo la mkutano, mswada huo uliahirishwa.

Wiki iliyopita, baada ya ripoti kuibuka kwamba White House ilikuwa inafikiria kutuma makombora ya Tomahawk na mifumo ya ulinzi ya anga aina ya Patriot kwenda Kyiv, Putin alimpigia simu Trump ambaye baadaye alitangaza uwezekano wa mkutano huko Budapest.

Siku iliyofuata, Trump alimkaribisha Zelensky Ikulu, lakini hawakufikia makubaliano yoyote, kufuatia mkutano ulioripotiwa kuwa na mvutano mkubwa.

Trump alikana kuwa anachezewa na Putin.

“Unajua, nimechezewa na watu hodari maisha yangu yote, lakini bado nimeibuka mshindi,” alisema.

Lakini Zelensky hakusita kueleza kile alichoona ni dalili ya mbinu za Urusi,

“Mara tu suala la silaha za masafa marefu lilipoanza kutoweka kwa Ukraine, Urusi mara moja ilipunguza hamu ya kufanya mazungumzo ya kidiplomasia,” alisema.

Ramani ya mashariki mwa Ukraine inayoonyesha mstari wa mbele ukipita katika mikoa minne

Ahadi iliyoyeyuka

Katika muda mfupi, Trump ameonyesha kuyumba kati ya kutuma silaha Ukraine, kupanga mkutano na Putin, na kumshinikiza Zelensky kwa faragha kukubali Urusi ichukue eneo la Donbas yote hata maeneo ambayo haijayateka kijeshi.

Hatimaye, amependekeza usitishaji vita kwa msingi wa mstari wa sasa wa mapambano pendekezo ambalo Urusi imelikataa.

Wakati wa kampeni mwaka jana, Trump aliahidi kuwa angekamilisha vita vya Ukraine “ndani ya saa chache tu”.

Tangu wakati huo, ameacha kauli hiyo, akisema kuwa kumaliza vita hivyo ni vigumu kuliko alivyoamini.

Ni miongoni mwa mara chache ambapo Trump amekiri mipaka ya uwezo wake na ugumu wa kutafuta amani wakati pande zote mbili hazipo tayari, wala haziwezi, kusalimu amri.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *