
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Emily Salley
- Nafasi, Mwandishi wa Michezo BBC
Vichapo vinne mtawalia, nafasi ya nne kwenye jedwali la Ligi Kuu England na pointi nne nyuma ya vinara Arsenal. Kuna kitu hakiko sawa kwa Liverpool.
Kwa timu ambayo ilitwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita, Liverpool wanaonekana wabovu nyuma, wavivu katika safu ya kati na wasio na umaliziaji kwenye safu ya ushambuliaji.
Tena ni baada ya meneja Arne Slot – kutumia karibu pauni milioni 450 kununua vipaji vipya.
Katika kipigo cha 2-1 Jumapili kutoka kwa Manchester United huko Anfield, wachezaji waliosajiliwa majira ya joto Florian Wirtz, Hugo Ekitike na Jeremie Frimpong – kwa jumla ya pauni milioni 214.5 – wote waliingia kutokea benchi.
Beki wa zamani wa Liverpool Stephen Warnock anasema, “si mara zote bei ya mchezaji, au jina la mchezaji, linainufaisha timu.”
BBC Sport imeangalia maswali muhimu ambayo Slot anapaswa kuyaweka sawa ikiwa Liverpool wanataka kuepuka kushindwa kwa mara ya tano mfululizo kwa mara ya kwanza tangu 1953.
Salah aachwe?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mohamed Salah amekuwa mtaji wa Liverpool kwa misimu minane iliyopita. Lakini, baada ya kufunga mabao 29 katika mechi 38 za ligi msimu uliopita, winga hiyo hajafunga magoli mengi msimu huu.
Salah hajafunga bao kwenye Ligi ya Premia tangu Septemba 14 alipofunga penalti ya dakika za lala salama na kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya Burnley. Pia hajafunga kwenye ligi tangu mechi ya ufunguzi ya Liverpool dhidi ya Bournemouth.
Ni mara ya kwanza kucheza mechi saba mfululizo za ligi kuu bila kufunga bao lisilo la penalti tangu ajiunge na Reds mwaka 2017.
Ukosefu wa magoli wa mchezaji huyo Mmisir mwenye umri wa miaka 33 ulionekana siku ya Jumapili alipokosa nafasi ya dhahabu mbele ya Kop wakati Liverpool walipokuwa wakisaka bao la kusawazisha.
Nyota wa Ligi Kuu England, Wayne Rooney ametilia shaka uchezaji wa Slah hasa kutokana na kusita kwake kurudi nyuma na kusaidia safu ya ulinzi.
Lakini Slot anajiamini vya kutosha kumwacha mchezaji ambaye amekuwa shujaa wa Liverpool?
Isak au Ekitike? Au wote?

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu England, amenunuliwa kwa pesa nyingi zaidi, pauni milioni 125 za Uingereza, matarajio yalikuwa makubwa baada ya Liverpool kumsajili Alexander Isak.
Kinyume na matarajio ya wengi, kazi haijawa rahisi kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Sweden tangu kuwasili kwake Merseyside.
Baada ya sakata la Newcastle na Liverpool kuhusu usajili wake, Isak alikosa mechi za maandalizi na mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya na anaonekana kushuka kiwango. Amecheza mechi saba za kwanza akiwa na Liverpool bila bao.
Mchezaji mwenzake aliyenunuliwa wakati wa majira ya kiangazi Ekitike aligonga vichwa vya habari kwa kufunga mabao matano katika mechi zake nane za kwanza.
Lakini mabao ya Mfaransa huyo yamekauka tangu alipotolewa kwa kadi nyekundu kwa kuvua jezi yake baada ya kufunga bao la dakika za mwisho dhidi ya Southampton kwenye Kombe la Carabao – kadi ya pili ya “kijinga” ya njano, kulingana na Slot.
Tangu wakati huo, Slot anamchezesha Isak katika namba tisa na Ekitike amekuwa akipata tabu kufunga akitokea benchi. Matatizo ya Isak yanaweza kumfanya bosi wa Liverpool kumrudisha Ekitike.
Mechi dhidi ya Manchester United, Isak aligusa mpira mara 19 pekee ndani ya dakika 71 uwanjani. Federico Chiesa, kwa kulinganisha, aligusa mara 23 na akatoa pasi ya bao la kusawazisha la Liverpool.
Je! Slot anapaswa kuendelea na Isak au kumuondoa? Au inawezekana kuwaweka Isak na Ekitike pamoja?
Safu ya kiungo ya Liverpool
Wirtz ni mchezaji mwingine aliyesajiliwa kwa pesa nyingi majira ya kiangazi ambaye hajaweza kutengeneza historia yake Liverpool.
Alisajiliwa kutoka Bayer Leverkusen Juni kwa ada ambayo inaweza kufikia pauni milioni 116, Wirtz – tofauti na Isak – alikuwepo katika maandalizi ya msimu mpya.
Lakini kiungo huyo mkabaji hajafunga bado akiwa na Liverpool, huku pasi yake pekee ya goli ni walipofungwa na Crystal Palace kwenye Ngao ya Jamii.
Wakati wa msimu uliopita alifunga mabao 10 na kutengeneza mengine 14 katika Bundesliga ya Ujerumani. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kwa kawaida aliwekwa upande wa kushoto.
Lakini msimu huu Slot anamtumia Wirtz katika nafasi ya nyuma ya washambuliaji.
Mabadiliko haya yanaonekana kuvuruga uimara wa safu ya kiungo inayoundwa na Ryan Gravenberch, Alexis Mac Allister na Dominik Szoboszlai, ambao walicheza mechi 22 za Ligi Kuu England pamoja huku Liverpool ikitwaa ubingwa.
Huku Wirtz akihangaika kuizoea nafasi hiyo, Slot amerudi kwa wachezaji wake watatu wa kiungo, na kumwacha benchi mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani.
Bado safu ya ushambuliaji ya Liverpool ni ya kivuvu na haina ubunifu. Wirtz, kwa kweli, amekuwa akitengeneza nafasi nyingi. Ametengeneza nafasi nyingi zaidi ndani ya dakika 90 kuliko mchezaji yeyote katika eneo hilo.
Je! Slot anapaswa kurejesha imani yake kwa Wirtz na kuwataka wachezaji wengine wafanye vyema zaidi kwa nafasi anazozitoa?
Marekebisho kwa mabeki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutokana na uwezo wake, kumpoteza Trent Alexander-Arnold baada ya kuhamia Real Madrid, kumeiathiri Liverpool.
Beki huyo wa kulia alifunga mabao 23 na alitoa pasi za mwisho 92 katika mechi 354 alizochezea katika klabu hiyo na Slot ameshindwa kuziba pengo hilo.
Ilifikiriwa Jeremie Frimpong angekuwa chaguo la kwanza, kutokana na kuwasili kwake kwa pauni milioni 29.5 msimu wa joto, lakini Mholanzi huyo amekuwa akishindana kukaa benchi na Conor Bradley na kiungo, Szoboszlai.
Upande huo wa kulia ndio ambapo Liverpool wamekuwa wazi zaidi, huku 38.1% ya mashambulizi yakitokea huko.
Frimpong na Bradley wote ni mabeki wa pembeni ambao wanapenda kupanda mbele, lakini hiyo ina maana kwamba mara nyingi huiacha wazi nafasi nyuma na kutumiwa wakati wa mashambulizi ya ghafla, na kukosekana kwa Salah kurudi nyuma kusaidia kunawaacha wazi zaidi.
“Hali ya beki wa kulia ni ya fujo,” anasema mshambuliaji wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza, Chris Sutton.
Pia kumekuwa na mabadiliko kwa upande mwingine wa safu ya ulinzi ya Liverpool, huku Andy Robertson akishushwa kuwa chaguo la pili baada kuwasili kwa beki wa kushoto Milos Kerkez kwa pauni milioni 40 kutoka Bournemouth.
Uchezaji wa Kerkez pia hauridhishi, Mhangaria huyo huondoka kwenye nafasi yake mara nyingi, na kumwacha beki wa kati Virgil van Dijk akiwa peke yake.
Je, Robertson anastahili nafasi nyingine? Na ni nani anayefaa zaidi kuwa beki wa kulia?
Walinzi wa wa kati?
Huku mabeki wa pembeni wakiwa wabovu, hilo linatoa mzigo zaidi kwa Van Dijk na Ibrahima Konate katikati. Na wao pia wameonekana kuwa hatarini, haswa dhidi ya mashambulizi ya ghafla.
Muda kama huu msimu wa 2024-25, Liverpool walikuwa wameruhusu mabao matatu pekee kwenye Ligi Kuu Engaland. Idadi hiyo imepanda hadi 11 msimu huu. Na wamefanikiwa kufunga mabao mawili pekee hadi sasa msimu huu. Wameruhusu mabao matano.
Makosa ya mtu binafsi yamekuwa ya gharama pia. Konate ameonekana kutotulia na mpira miguuni na amefanya makosa kwa mabao yote mawili ya Bournemouth katika mechi yao ya kwanza ya msimu.
Slot atawezaje kurekebisha safu ya nyuma ya Liverpool kabla ya kuwagharimu mabao na pointi zaidi?