Israel yatambua miili ya Mateka, Vance akutana na NetanyahuIsrael yatambua miili ya Mateka, Vance akutana na Netanyahu

Taarifa hiyo imesema miili iliyotambuliwa ni ya Arie Zalmanovich na Tamir Adar. Shirika la Msalaba Mwekundu limesaidia kusafirisha miili hiyo, ambayo ilikuwa imehifadhiwa kwenye masanduku maalum ya kubebea maiti, na kuikabidhi kwa jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mateka hao wawili waliuawa katika eneo la Kibbutz Nir Oz mnamo Oktoba 7, 2023, wakati wanamgambo wa Hamas walipovamia kusini mwa Israel, tukio lililochochea mzozo wa sasa wa Mashariki ya Kati, ambao umeendelea kwa zaidi ya miaka miwili.

Tangu kutekelezwa kwa makubaliano ya usitishaji mapigano Oktoba 10 mwaka huu, mabaki ya mateka 15 waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo wa Kipalestina yamerudishwa Israel. Hata hivyo, miili mingine 13 bado inahitaji kutambuliwa ili kurejeshwa nyumbani.

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano hayo ya usitishaji mapigano, ambapo sharti jingine linalosubiri kutekelezwa, ni Hamas kuweka silaha chini, kisha vikosi vya usalama vya kimataifa kupelekwa Gaza, ili kuamua mustakabali wa uongozi wa eneo hilo lililokuwa chini ya udhibiti wa Hamas.

Miili ya wapalestina iliyorejeshwa nyumbani kuzikwa Gaza

Wakati huo huo, maziko ya zaidi ya miili 50 ya Wapalestina iliyorejeshwa Gaza kutoka Israel, yanatarajiwa kufanyika leo katika makaburi ya Deir al-Balah. Israel bado inashikilia miili ya takriban 165 ya Wapalestina waliokufa wakiwa magerezani.

Miili ya waplestina iliyorejeshwa nyumbani kutoka Israel waagwa Gaza
Maziko ya zaidi ya miili 50 ya Wapalestina iliyorejeshwa Gaza kutoka Israel, yanatarajiwa kufanyika katika makaburi ya Deir al-Balah.Picha: Abdel Kareem Hana/AP Photo/picture alliance

Haya yanajiri wakati Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, akikutana na Waziri Mkuu Netanyahu pamoja na Rais wa Israel, Isaac Herzog, kwa mazungumzo kuhusu amani ya Gaza. Vance ameandamana na wajumbe maalum wa Marekani kwa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff na Jared Kushner. Vance amesema ana matumaini makubwa kwamba makubaliano ya amani Gaza yataendelea kutekelezwa ipasavyo, lakini akatahadharisha kuwa mambo sio rahisi.

“Tumeingia wiki moja ya mpango wa amani wa Trump Mashariki ya Kati naweza kusema mambo yanakwenda vizuri kuliko nilivyotarajia. Lakini pia lazima tujue kwamba hii ni hali ngumu ngumu sana. Tunafanya kazi pamoja na serikali ya Israel kuanza mpango wa kuijenga upya Gaza kutekeleza amani ya muda mrefu na kuhakikisha kuwa kuna vikosi vya usalama Gaza ambavyo havihusishi wamarekani vinavyoweza kuhakikisha amani inakuwepo huko kwa muda mrefu,” alisema Vance.

ICJ kutoa uamuzi kuhusu wajibu wa Israel kwa misaada ya Gaza

Wakati uo huo Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa (ICJ) inatarajiwa kutoa maoni yake kuhusu wajibu wa Israel kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yanayotoa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Maoni hayo, yaliyoombwa na Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba, yanatarajiwa kubainisha wazi kiwango cha ulinzi ambacho mataifa yanapaswa kutoa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa duniani kote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *