Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa mauaji ya vijana wanne ambao miili yao iliokotwa kando mwa barabara mkoani Pwani, wazazi wao wamesema yote yaliyotokea wanamuachia Mungu.

Mbali ya hayo, mashuhuda wameibua mapya wakidai tukio hilo liliwahusisha baadhi ya askari na sungusungu, ambao kauli yao ya kwanza walipofika kwenye nyumba walimokuwamo vijana hao ilikuwa: “Chukueni mapanga yao.”

Vijana hao, watatu wakiwa madereva wa pikipiki na mmoja wa bajaji wanadaiwa kuchukuliwa nyumbani kwao Tabata kwa Swai, wilayani Ilala, Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Oktoba 14, 2025.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, Oktoba 16, 2025 lilieleza lilipokea taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kidimu kwamba, maeneo ya Kidimu- Vingunguti, wilayani Kibaha, mkoani humo imeonekana miili ya watu wanne wasiojulikana ikiwa pembezoni mwa barabara inayotoka Mapinga kuelekea Kibaha.

Miili hiyo ilipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kabla ya kutambuliwa na kuchukuliwa na familia zao kwa ajili ya mazishi.

Miili hiyo ni ya Mikidadi Mikidadi (21) na Hassan Jumanne (21), wakazi wa Tabata Chang’ombe, Fadhili Hiyola (19), mkazi wa Vingunguti na Abdalla Nyanga (21), maarufu Dulla Nditi, mkazi wa Tabata Kisukuru.

Kwa mujibu wa familia za marehemu hao, vijana hao walichukuliwa na watu watatu waliokuwa wameficha nyuso zao kwa kofia nyeusi, huku mmoja wao akiwa na pingu.

Akizungumza na Mwananchi jana Oktoba 21, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema uchunguzi unaendelea na wamezungumza na wazazi lakini hawajapata maelezo ya kutosheleza kuhusu shughuli za vijana wao.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, tuliwahoji wazazi kuhusu shughuli maalumu za watoto wao, lakini hawatoi maelezo yaliyonyooka, hivyo tumeamua kufanya uchunguzi kwa njia zetu wenyewe,” amesema.

Tunamuachia Mungu

Wakati Jeshi la Polisi likitoa kauli hiyo, wazazi wa Abdalla, Hassan na Mikidadi wamesema wamemuachia Mungu suala hilo kwa sababu hawajui hata kama watafungua kesi, ni nani wa kumshtaki.

Sauda Ramadhani, mama wa marehemu Abdalla amesema hawana mpango wa kufungua kesi zaidi ya kumuachia Mungu, akieleza uchunguzi wa polisi unaendelea kama ambavyo wenyewe wameeleza.

“Tunamuachia Mungu maana hata tukifungua kesi mtoto hawezi kurudi, pia tukisema tufanye hivyo hatujui tunamshitaki nani,” amesema.

Nasri Wamba, baba mlezi wa Hassan Jumanne amesema watakaa kikao cha familia kujadiliana cha kufanya, lakini wanamuachia Mungu atakayeamua cha kufanya.

Mama aliyekataa kutaja jina lake, aliyejitambulisha kuwa ni mzazi wa Mikidadi amesema:

“Kwa sasa hata baba yake hayupo vizuri kutokana na msiba wa mwanaye, ukimweleza kuhusu ufuatiliaji wa mambo ya kesi utakuwa unamchanganya.”

Nilimuona sungusungu

Aisha Abdallah, dada wa marehemu Dulla amesema siku ya tukio saa sita usiku wa Oktoba 14, alikuwa kwa mdogo wake akiwa na marafiki zake pamoja na wale wa kaka yake.

Amesema Dulla alikuwa akiishi na mkewe na mtoto wake, lakini marafiki zake Fadhili na Mikidadi walikwenda kuwatembelea, kwa kuwa nyumba wanayoishi alipanga Dulla na Hassan.

Aisha amesema wakiwa nyumbani hapo wakiendelea na maongezi, Dogo Panya (jina lautani) alipiga simu akaeleza amepita kununua chipsi lakini atakwenda nyumbani hapo.

“Baada ya kumaliza kula nilikwenda chumbani nikiwa na wifi na mtoto wake mdogo, chumba kingine nilimuacha Dulla, marafiki zangu na wa kwake wakiendelea na stori,” amesema.

Aisha amesema akiwa kitandani usiku alisikia mlango ukigongwa kwa nguvu, alipotaka kufungua wifi yake alimkataza, lakini yeye akafungua.

Amedai kuwa, alikutana na askari aliyemuelekezea silaha, hivyo alirudi kinyumenyume hadi kitandani.

“Kwa woga nikachukua simu ili nimpigie mama kuwa tumevamiwa, alinipokonya simu. Nilimuomba kuwa sipigi tena simu anirudishie lakini alikataa,” amesema.

Amesema mtu huyo alimzuia ili asijue kinachoendelea chumba kingine, huku akichungulia kama wengine wamemaliza kilichowapeleka.

Aisha amesimulia kuwa, mtu huyo alitoka nje kisha akaitupa chini simu yake na alipoinama kuiokota alimuona sungusungu mmoja mrefu, mweusi akiwa ameshika rungu, ambaye aliongozana na watu hao walipokuwa wakiondoka.

Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Mayasa, amesema watu waliofika nyumbani hapo walikuwa takribani saba na kauli yao ya kwanza ilihusu mapanga na simu.

“Walipoingia neno lao la kwanza walisema toeni mapanga yao na chukueni simu zao wote. Baada ya hapo waliwafunga mashati juu ya kichwa kama kuni, walituamuru sisi tulale kifudifudi, tujifunike kwa mashuka,” amesema Mayasa.

Amedai simu zilizochukuliwa zilikuwa sita, tatu zikiwa simu janja na tatu nyingine ni za kawaida.

Hata hivyo, amesema mapanga yaliyodaiwa yachukuliwe ndani ya nyumba hiyo hayakuwepo hivyo waliondoka na simu pekee.

Baada ya kuchukua simu hizo, amesema watu hao waliondoka na vijana hao wanne kabla ya Dogo Panya hajafika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, Dogo Panya hakuwapo katika tukio hilo kwa sababu alichelewa kufika, hivyo walikutana naye njiani walipokuwa wanakwenda nyumbani kwa wazazi wa Dulla, Mtaa wa Banebane ulioko Kisukuru.

Sauda, mama wa Dulla amesema watoto wake walifika nyumbani kwake wakamueleza mwanaye na marafiki zake wamechukuliwa na watu wenye silaha zaidi ya 10.

Amesema kutokana na taarifa kutolewa usiku walisubiri kupambazuke ili wajue wapi pa kuanzia kuwatafuta.

“Walivyoniambia ndugu zao wamechukuliwa niliwaambia saa hii ni usiku, tutaanzia wapi? Tunatakiwa kusubiri mpaka asubuhi. Siku hiyo tulianza kuwatafuta kwenye vituo vya polisi vya karibu,” amesema.

Amesema baada ya kuzunguka na kuwakosa, saa saba mchana alimpigia simu mama yake Hassan na Mikidadi, akawapa taarifa ya kuchukuliwa kwa watoto na vituo walivyozunguka ili na wao wazungukie vingine.

Mama huyo amesema baada ya kuzunguka akiwa amerudi nyumbani, aliwaeleza ndugu wengine waende Kituo cha Polisi Gogoni, lakini walipofika eneo la Kwa Mkuwa walikutana na mtu aliyewahoji wanakoelekea maana walikuwa kundi.

“Walikutana na dereva wa bajaji akawauliza mnakwenda wapi? Walimwambia hali halisi, dereva huyo aliwaambia amesikia kuna watu wanne wameokotwa Kibaha na wamepelekwa Tumbi,” amesema.

Amesema binti yake alimpigia simu akamueleza jambo hilo, hivyo aliwapigia wazazi wengine (mama wa Hassan na Mikidadi).

Amesema walipanda pikipiki hadi Kibaha lakini kutokana na woga, waliwatuma vijana waliokwenda nao kuingia mochwari kutambua miili iliyobainika kuwa ni ya watoto wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *