
Dar es Salaam. Shomari Kapombe na Fiston Mayele hawajakutana uwanjani tangu Mayele alipojiunga na Pyramids FC ya Misri mwaka 2023 akitokea Yanga.
Hata hivyo wawili hao sasa wamejikuta wakikutanishwa lakini nje ya uwanja baada ya wote kuteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano ya Klabu za Afrika wa mwaka 2025.
Katika orodha iliyotolewa na CAF leo ya wachezaji 10 wanaowania tuzo hiyo, Mayele na Kapombe wametajwa.
Mchango ambao wawili hao wameutoa kwa klabu zao katika msimu uliopita umeonekana kuwabeba na kuwafanya waingie katika kinyang’anyiro hicho.
Mayele aliiongoza Pyramids FC kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambapo aliifungia mabao sita yaliyomfanya awe Mfungaji Bora.
Wiki iliyopita, Mayele tena aliiongoza Pyramids FC kutwaa taji la CAF Super Cup akifunga bao pekee la ushindi dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Kapombe alitoa mchango mkubwa kuiwezesha Simba kutinga hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika akicheza zaidi ya asilimia 90 ya mechi zote.
Pyramids FC imeonekana kutamba kwa kutoa idadi kubwa ya wachezaji kwenye orodha hiyo ya nyota 10 wanaowania tuzo hiyo.
Timu hiyo imetoa wachezaji wanne ikifuatiwa na RS Berkane ambayo imetoa wachezaji wawili.
Ukiondoa Mayele na Kapombe, nyota wengine wanaowania tuzo hiyo ni Ismail Belkacem, Blati Toure, Issoufou Dayo, Emam Ashour, Ibrahim Adel, Mohamed Hrimat, Mohamed Chibi na Oussama Lamlioui.