Dar es Salaam. Nyota wa Bongo Fleva, Billnass amesema mapenzi yake kwa mkewe Nandy yaheshimiwe huku akiwachana wanaomfuatilia kwa mabaya katika ndoa yao.
Billnass anasema watu wengi wamekuwa wakidhani uhusiano wake na Nandy ni kwa sababu ya pesa za mwanadada huyo anayefanya vizuri katika Bongo Fleva na si mapenzi na hapa ameamua kuweka wazi kila kitu ikiwamo tetesi za kuachana.
Akizungumza na Mwananchi Billnass anasema kuhusu ndoa yao inawaumiza wengi na wanatamani waachane na ndiyo maana wanaleta maneno mengi, lakini anachojua wao wako vizuri na hazuii watu kuongea.
Billnass anayetamba na nyimbo nyingi kama Boda, Magetoni, Maokoto, Chafu Pozi, Ligi Ndogo na nyingine nyingi aliiambia safu hii midomo ya watu siku zote haiishi kusema na wanatumia mitandao kujazana uwongo jambo ambalo hajali.
“Hivi kwa nini watu hupenda kusema nimefata pesa kwa Nandy? Yaani wananichukuliaje? Ujue huwa nawashangaa sana watu hao, halafu nifuate pesa kwa Nandy kwani amekuwa benki? Halafu watu hao wanaosema hivyo ni wazi watakuwa masikini sana kwa sababu sijawahi ona Nandy kama ana pesa sana, wao sasa wanaomuona ana pesa maana yao wana hali ya chini.”
Kafuata upendo
Anaendelea kusema; “Sasa mimi watu kama hao nawezaje kujibishana nao wakati nimeshajua tatizo lao ni kutokana na kipato chao na kumwona Nandy ana pesa. Embu watu tuheshimiane jamani mimi nimefuata upendo kwa Nandy na sio pesa, pesa hata mimi ninazo.”
Walikotoka
Anasema walikutana katika kazi yao hiyo na wamepitia mengi tangu mwanzo.
“Kwa mara ya kwanza ilikuwa katika Tamasha la Fiesta lililofanyika mkoani Mbeya mwaka 2016, ila tumepitia mengi sana hadi kufikia hatua ya kufunga ndoa, yaani kiufupi tulianza kusemwasemwa kabla hata ya kufunga ndoa.”
Ishu ya kuachana, kurudiana
Alipoulizwa kuhusu kuachana na kurudiana kwa madai ya usaliti Billnass alicheka na kufunguka;
“Lini tumeachana? (Kicheko) hayo ni madai tu kama madai mengine, sasa kwa nini tuachane? halafu kwa nini tusalitiane? Hakuna kitu kama hicho bwana na ndiyo maana hukusikia tumezunguza sehemu tumeachana.”
Tofauti ya Nandy na wapenzi wa zamani
“Nandy ni mtu ambaye anajituma sana. Robo tatu ya maisha yake ni mwanamke anayefanya kazi sana. Muda mwingi sana anafikiria maisha na ni mwanamke mwelewa sana, pia ana wivu sana.”
Ushauri wake kwa mkewe
“Kwanza asiwe na makundi mengi ya marafiki, asiwe mzungumzaji wa mambo yetu ya familia, apende kusali, asiwe na hasira na kitu akikisikia wala kusemwa, ndiyo maana kila siku huwa namwambia huwezi kuwa na jina kubwa ushindwe kupitia mambo kama hayo, hivyo nampa moyo tu aendelee kupiga kazi.”
Nandy yuko hivyo kweli?
“Ndiyo maana hujawahi msikia akiwa na tabia hizo, mimi nimejibu kutokana na swali lako tu kuhusu ushauri.”
Vipi kuhusu kushikiana simu, haileti ugomvi?
“Hakuna kabisa na sisi kila mmoja anashika simu ya mwenzake muda wowote anaotaka, anajua namba yangu ya siri na mimi ninajua yake, ndiyo maisha yetu.”
Mwambie maneno matamu Nandy
“Nampenda sana na nitaendelea kumpenda hadi siku ninapelekwa kaburini.”