
Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza imeripoti kuwa ni malori 986 pekee ya misaada yaliyoingia katika eneo hilo linalozingirwa tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya Harakati ya Mapambano ya Palestina (Hamas) na utawala wa Israel tarehe 10 mwezi huu.
Ofisi hiyo imeeleza kuwa malori ya misaada ya kibinadamu yaliyowasili Gaza ni sawa na asilimia 15 tu ya malori 6,600 yaliyotazamiwa kuwasili katika eneo hilo hadi kufikia tarehe 20 mwezi huu wa Oktoba.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza imesema kuwa msafara huo ulikuwa na malori 14 ambayo yalikuwa yamepakia gesi ya kupikia huku malori mengine 28 yalikuwa yamebeba mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme wa sola ambayo hutumika katika viwanda vya kuoka mikate, kuwashia majenereta, hospitalini na katika shughuli nyingine.
“Ugavi unaendelea kuwa duni baada ya miezi kadhaa ya vizuizi na uharibifu wa makusudi kufuatia vita vya mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza,” imeeleza taarifa ya Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza.
Aidha imeelezwa kuwa wastani wa idadi ya malori ya misaada ambayo yamekuwa yakiingia Ukanda wa Gaza kila siku tangu kuanza usitishaji vita ni 89, idadi ambayo ni chini ya malori 600 yaliyoafikiwa hapo awali.
Taarifa ya Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza imesema kuwa hali hii inathibitisha kuendelea sera ya Israel ya mbinyo, njaa na utumiaji mabavu dhidi ya raia milioni mbili wa Gaza.