Kupitia mafunzo, huduma za kifedha, na upatikanaji wa masoko, wanawake wanawezeshwa kiuchumi na kijamii. Tafiti zinaonesha kuwa kufuta pengo la kijinsia katika kilimo kunaweza kuongeza pato la dunia kwa asilimia 1. Nchini Rwanda, miradi kama R-YES imewezesha wanawake vijana kuanzisha biashara za kilimo na kutoa ajira.
Adelaide ni mkulima mdogo kutoka Rwanda, ambaye maisha yake yamebadilika kwa msaada wa IFAD. Hii ni sehemu ya dhamira ya IFAD, kupitia mpango wa Agriconnect wa Benki ya Dunia, kubadili maisha ya wakulima wadogo milioni 70 ifikapo 2030. Anasema,
Adelaide, Mkulima mdogo kutoka Rwanda, ambaye maisha yake yamebadilika kwa msaada wa IFAD
“Watu wengi hufikiri kilimo ni kazi ya kuchafuka tu, lakini kwa kweli unaweza kulima ukiwa ofisini kwa sababu ya teknolojia tunayoijaribu kama wanavyofanya katika nchi za Ulaya ambazo zina kilimo kilichoendelea. Kilimo hiki cha kisasa kinakuwezesha kupata taarifa zote kuhusu kinachoendelea shambani kwako.”
Dagmawi Habte-Selasie, Mkurugenzi wa IFAD huko Rwanda, anasisitiza umuhimu wa kuweka mazingira yanayorahisisha wakulima kuunganishwa na mifumo ya chakula. Anasema:
“Tunaweka mazingira rahisi kwao kuingia katika mifumo hii ya chakula, badala ya kujaribu kutoka vijijini kwenda mijini au hata kuvuka kwenda mabara mengine. Kwa kufanya hivyo, tunawapa fursa ya kubadili maisha yao, kuboresha maisha ya jamii zao, na kwa kweli kusaidia katika kuendeleza nchi zao kwa ujumla.”
Bi Adelaide anatamatisha kwa kusema,
“Sasa hivi, kupitia greenhouse yetu, tunaweza kuajiri watu watano au sita. Lakini katika siku zijazo, tunapanga kutoa ajira kwa watu wengi zaidi, tukifikia mia moja au zaidi, endapo mambo yataendelea kwenda vizuri.”
Bidhaa za wakulima wadogo ambazo IFAD imewekeza zimeonesha ongezeko la wastani la asilimia 34 katika mapato yao, asilimia 35 katika uzalishaji, na asilimia 34 katika upatikanaji wa masoko, kulingana na tathmini ya hivi karibuni ya IFAD kuhusu miradi mbalimbali.