KOCHA Mkuu wa Bunda Queens, Alley Ibrahim, amesema kikosi chao kwa sasa kimeshakomaa na kupata uzoefu wa mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, hivyo msimu huu kiko tayari kwa ushindani ili kumaliza ndani ya nafasi nne za juu.

Huu ni msimu wa tatu kwa timu hiyo yenye maskani yake wilayani Bunda Mkoa wa Mara baada ya kupanda daraja na kuanza kushiriki Ligi Kuu msimu wa 2023-2024.

Pazia la ligi hiyo litafunguliwa rasmi Novemba 6, 2025, ambapo kikosi hicho kitaanzia ugenini dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo na Ngao ya Jamii, JKT Queens kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar, saa 10:00 jioni.

Mechi hiyo itakuwa ya tano kwa timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu tangu mwaka 2023, ambapo katika msimu wa 2023-2024, JKT Queens ilishinda mabao 4-0 ugenini na 2-1 nyumbani. Msimu uliopita, maafande hao walilazimishwa sare ya 1-1 ugenini na kushinda 3-0 nyumbani.

Akizungumzia mechi hiyo, Ibrahim alisema licha ya ubora wa JKT Queens, lakini wamejiandaa vyema kuwakabili huku wakiyatumia mashindano ya Ngao ya Jamii kuwasoma na kujua udhaifu wao.

“Tumejiandaa vizuri kuanza msimu ukizingatia ni wa tatu tangu tupande Ligi Kuu, tumejifunza vitu vingi kuhusu mpira wetu wa kike na mpaka sasa tunaendelea na maandalizi yetu,” alisema Ibrahim.

Aliongeza:  “Tunafungua msimu na mabingwa watetezi ambao ni timu bora katika ukanda wetu, hivyo tumewaandaa wachezaji kukabiliana na ubora huo na tumetumia mechi za Ngao ya Jamii kuwafuatilia wanavyocheza kujua ubora wao ulipo na kutazama udhaifu wao.”

Alisema baada ya kusuasua misimu miwili iliyopita kutokana na uchanga wao kwenye Ligi Kuu, msimu huu wamejipanga kivingine kwani wanataka kufanya vizuri wakijiwekea malengo ya kumaliza ndani ya nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi.

“Msimu huu naamini nina timu nzuri, nawaamini mabinti zangu, nina matumaini tutafanya vizuri,” alisema Ibrahim.

Aliongeza: “Timu yetu haijafanya usajili wa mchezaji hata mmoja bali tumepandisha wachezaji kutoka kituo chetu cha Bunda Queens Program. Pia, hatuna mchezaji hata mmoja wa kigeni.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *