
TIMU ya Fufuni kutoka kisiwani Pemba, imeendelea kuwa timu iliyopanda daraja msimu huu kushiriki Ligi Kuu Zanzibar kuwa na matokeo mazuri zaidi ya nyingine hadi sasa baada ya kuvuna alama kumi ikishuka dimbani mara nne ikikaa katika Top 4 ya msimamo wa ligi hiyo.
Kabla ya mechi za jana Jumatano, Fufuni ilikuwa katika nafasi ya tatu ikikusanya pointi kumi sawa na KVZ iliyokuwa ya nne ambayo ilicheza na Mafunzo jana jioni. Kinara ni Uhamiaji yenye pointi 12 ikifuatiwa na Malindi (11).
Fufuni ilianza ligi kwa kucheza mechi nne mfululizo ugenini na kufanikiwa kukusanya pointi saba ikishinda mbili, sare moja na kupoteza moja kabla ya juzi kushinda nyumbani.
Matokeo ya mechi hizo tano ilizocheza Fufuni hadi sasa ni; Kipanga 1-3 Fufuni, Mafunzo 1-1 Fufuni, Malindi 2-0 Fufuni, Zimamoto 0-3 Fufuni na Fufuni 1-0 Polisi.
Wakati Fufuni ikifanya vizuri, timu nyingine tatu zilizopanda daraja ni Polisi inayoshika nafasi ya sita kwa pointi sita, New King ya 11 ikikusanya pointi nne na New Stone Town inaburuza mkia bila ya pointi.
Fufuni hadi sasa imefanikiwa kuteka hisia za mashabiki na wadau wa soka kisiwani hapa kwa namna inavyopambana kusaka ushindi katika mechi zake.
Ukiweka kando mbwembwe na madoido ya kocha mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohammed wakati akishangilia timu hiyo inapopata ushindi, wachezaji wa kikosi hicho wamekuwa na utulivu mkubwa ndani ya uwanja kwani hata wakitanguliwa kufungwa bao, hawatoki mchezoni.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Fufuni, Suleiman Mohammed amesema malengo yao msimu huu wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Zanzibar wanataka wasirudi walipotoka.
Amesema licha ya ratiba ya ligi kubana, lakini wanapambana kuhakikisha ugenini wanafanya vizuri na nyumbani hakuna mgeni atakayechukua pointi yoyote.