
Serikali ya Israel imetangaza leo kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,Marco Rubio, atakutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, siku ya Ijumaa mjini Tel Aviv. Ziara hiyo inafanyika wakati utawala wa Rais Donald Trump ukijaribu kuimarisha makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, yaliyofikiwa zaidi ya wiki moja iliyopita.
Mapema leo, Netanyahu akizungumza mbele ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ambaye yuko ziarani nchini humo, alisema Israel inasimamia usalama wake yenyewe na si “mlinzi wa Marekani.” Aliongeza kuwa serikali yake itaendelea kupambana na Hamas na kuzuia tishio lolote jipya katika Ukanda wa Gaza.
Netanyahu amesema “tumefanikiwa kufanya mambo mawili. Kuweka kisu kwenye koo la Hamas — huo ulikuwa ni mchango wa kijeshi wa Israel. Na juhudi nyingine ilikuwa kuwatenga Hamas katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, jambo ambalo naamini rais wa Marekani pamoja na timu yake walilifanya vyema sana. Kwa hiyo, mambo hayo mawili ndiyo yaliyopelekea kuachiliwa kwa mateka. Hakuna aliyedhani tungeweza kuwatoa.“
Katika shambulio la Oktoba 7, 2023, wanamgambo wa Hamas waliwaua takriban watu 1,200, wengi wao wakiwa raia, na kuchukua mateka 251, tukio lililoanzisha vita vinavyoendelea hadi sasa.