Tommy Piggott, Naibu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema siku ya Jumanne kwamba Marco Rubio Waziri wa Mambo ya Nje, katika mazungumzo yake na Mohammad Shia Al-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, ametoa wito wa kupokonywa silaha makundi ya muqawama ya nchi hiyo akidai kuwa ni tishio kwa maslahi ya Washington na Baghdad.

Ikiwa ni katika kutetea maslahi na sera za Washington, msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ametoa wito wa kupokonywa silaha makundi ya muqawama ya Palestina na Lebanon, yakiwemo ya Hamas na Hizbullah, kwa manufaa ya Israel, licha ya kuwa makundi ya muqawama ya Iraq ni huru na yanajitegemea. Kwa kukariri madai kuhusu ushawishi wa kieneo wa Iran na uhusiano wake na makundi hayo, ametaka kupokonywa silaha makundi yote ya muqawama ya Iraq na kusema: “Rubio anasisitiza ulazima wa kuwapokonywa silaha wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwa sababu makundi ambayo yanadhoofisha mamlaka ya Iraq, yanatishia maisha na maslahi ya raia wa Marekani na Iraq, na kupora rasilimali za Iraq kwa manufaa ya Iran.”

Piggott amedai: “Waziri wa Mambo ya Nje anasisitiza dhamira ya Marekani ya kushirikiana kwa karibu na washirika wa Iraq ili kuendeleza maslahi ya pamoja kati ya Washington na Baghdad, ikiwa ni pamoja na kulinda mamlaka ya Iraq, kuimarisha utulivu wa eneo na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi mbili.”

Ili kulinda maslahi yake nchini Iraq na kuhakikisha usalama wa Israel, Marekani imekuwa ikitoa madai yasiyo na msingi na ya mara kwa mara dhidi ya muqawama wa Iraq na kutaka makundi hayo yapokonywe silaha. Kwa ujumla, nia ya Marekani katika kuyapokonywa silaha makundi ya muqawama nchini Iraq imeibuliwa kwa madai ya kupunguza ushawishi wa Iran nchini Iraq, kudhamini usalama wa majeshi ya Marekani na kuimarisha mamlaka ya kujitawala serikali ya Iraq. Hata hivyo, nyuma ya madai na sababu zinazotamkwa hadharani na Marekani katika uwanja huu, kuna malengo makubwa zaidi ya kistratijia yanayoonyesha ushindani kati ya Marekani na Iran katika eneo, ikiwa ni pamoja na:

– Kudhoofisha “mhimili wa muqawama”: Makundi ya muqawama nchini Iraq ni moja ya nguzo muhimu za mhimili wa muqawama na mapambano unaoongozwa na Iran katika eneo. Kupokonywa silaha makundi hayo bila shaka kutadhoofisha uwezo wa kieneo wa Iran wa kuzuia uchokozi wa adui na kubadilisha mizani ya nguvu kwa manufaa ya Marekani na washirika wake wa eneo kama Israel.

Marco Rubio, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani

– Kuimarishwa ramani ya “Mashariki ya Kati Mpya”: Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba msukumo wa kupokonywa silaha ni sehemu ya mpango mkubwa zaidi wa kuunda upya utaratibu wa usalama wa eneo hili kwa jina la “Mashariki ya Kati Mpya”. Mpango huu hatimaye unaweza kudhoofisha umoja wa nchi kama vile Iraq na kupunguza vizuizi vya kupanuka ushawishi wa utawala wa Kizayuni katika eneo.

– Kubuni uwiano katika mkesha wa kujiondoa: Kwa kuzingatia mwanzo wa mazungumzo ya kuondoka majeshi ya Marekani huko Iraq, Washington inajaribu kuhakikisha kwamba washirika wake wa kieneo (hasa Wakurdi wa kaskazini mwa Iraq) hawatakuwa katika nafasi dhaifu kabla ya kuondoka nchini humo. Kupokonywa silaha kwa makundi ya muqawama ya Iraq ni muhimu kwa mtazamo wa Washington kuhusu suala hili.

Sera hii ya Marekani imekabiliwa na hisia kali na inaweza kusababisha madhara makubwa ya kiusalama ikiwa ni pamoja na:

– Radiamali kali ya makundi ya muqawama: Viongozi wa makundi haya wamekataa kabisa ombi lolote la kukabidhi silaha na kulitaja kuwa la ” Kizayuni na Kimarekani”. Wanazichukulia silaha zao kama amana waliyoitumia katika kulinda nchi na maeneo matakatifu wakati jeshi la Iraq lilipolemewa na magaidi wa Daesh.

– Kuongezeka mvutano wa ndani nchini Iraq: Suala hili limeiweka serikali ya Mohammed Shia al-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, katika hali ngumu sana. Kwa upande mmoja, yuko chini ya mashinikizo makubwa kutoka kwa Marekani, na kwa upande mwingine, hawezi kupuuza matakwa ya makundi ya muqawama. Mvutano huu unaweza kuibua mgawanyiko wa kisiasa mjini Baghdad.

– Hatari ya kurujea ugaidi: Wachambuzi wengi wanaonya kwamba kudhoofishwa makundi hayo, ambayo yana historia ndefu na muhimu ya mapambano dhidi ya Daesh, kunaweza kudhoofisha muundo mzima wa ulinzi wa Iraq na kufufua ugaidi wa Kitakfiri na hivyo kukaririwa tena kwa hali hatari iliyoshuhudiwa nchini humo mwaka 2014.

Muhtasari

Kwa ujumla, ombi la Marekani la kupokonywa silaha makundi ya mapambano na muqawama nchini Iraq sio ombi la usalama la kawaida tu. Takwa hilo ni dhihirisho la ushindani mkubwa wa kijiopolitiki uliopo kati ya Iran na Marekani nchini Iraq. Kupitia mashinikizo hayo, Washington inataka kulinda usalama wa vikosi vyake na wa washirika wake, kudhoofisha muqawama wa kieneo na kubuni mpango mpya wa usalama wa Asia Magharibi kwa msingi wa maslahi ya Washington na Tel Aviv. Hata hivyo, mafanikio ya mkakati huu yanakabiliwa na mambo magumu, ikiwa ni pamoja na upinzani mkali wa makundi ya muqawama ya Iraq, maamuzi ya serikali ya Iraq na matukio ya baadaye katika eneo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *