Zaidi ya shakhsia 450 wa Kiyahudi kutoka duniani kote wametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na viongozi wa kimataifa kuuwekea vikwazo utawala wa Israel kutokana na mauaji ya kimbari “yasiyokubalika” katika Ukanda wa Gaza.

Ripoti iliyotolewa jana Jumatano na gazeti la The Guardian la Uingereza imesema: Katika barua ya wazi, waliotia saini, wakiwemo maafisa wa zamani wa utawala wa Israel, waandishi na wasanii walioshinda tuzo, wametaka Israel iwajibishwe kutokana na sera zake katika eneo la pwani pamoja na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Waliotiwa saini barua hiyo wameonya kwamba mienendo ya Tel Aviv imekiuka sheria za kimataifa na kanuni zilezile zilizoundwa ili kuzuia ukatili wa watu wengi.

Miongoni mwa waliotia saini baraka hiyo ni spika wa zamani wa Knesset (Bunge la Israel) Avraham Burg, mpatanishi Daniel Levy, waandishi Michael Rosen na Naomi Klein, mtengenezaji wa filamu Jonathan Glazer, na waigizaji Wallace Shawn na Ilana Glazer.

Takwa hilo la pamoja limesisitiza kuwa serikali za nchi mbalimbali zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kuzuia madhara zaidi kwa Wapalestina.

Barua hiyo imeyahimiza mataifa yote kuheshimu maamuzi ya mahakama za kimataifa, kusitisha upelekaji wa silaha huko Israel, kutekeleza vikwazo dhidi ya utawala huo na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.Shakhsia hao wa Kiyahudi pia wamepinga “madai ya uongo yanayotolewa dhidi ya wale wanaotetea amani na haki kuwa wana chuki dhidi ya Mayahudi.”

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, utafiti wa hivi majuzi ulionukuliwa na gazeti la The Guardian umeonyesha kuwa asilimia 61 ya Wayahudi wa Marekani wanaamini kuwa Tel Aviv ilifanya uhalifu wa kivita dhidi ya Wapalestina, huku asilimia 39 wakisema inafanya mauaji ya kimbari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *