Utamaduni wa kampuni ni kanuni zinazounda mazingira ya kijamii na kisaikolojia ndani ya taasisi fulani. Kanuni hizo ndizo zinazojenga msingi wa mtazamo wa namna mambo yanavyofanyika ndani ya kampuni au shirika husika.

Utamaduni huo unaweza kutokana na mambo kadhaa; kwa mfano, taratibu ilizojiwekea kampuni, aina ya wafanyakazi walio nao, eneo ilipo kampuni hiyo, biashara kuu wanayofanya, malengo waliojiwekea, Sheria na kanuni za sekta iliyopo na mengine mengi.

Kwa ujumla utamaduni huo unabeba mambo kadhaa kwa mfano maadili ya wafanyakazi, mazoea, uongozi na tabia zao, namna ilivyo mtindo wa kiuongozi na usimamizi, mawasiliano na ushirikiano baina ya wafanyakazi, na wateja na mengine.

Namna ya utamaduni huo utakavyokuwa mzuri ndio unaweza kuchangia ufanisi, uchapakazi, ubunifu, na ustawi wa kampuni husika na mwishowe utaweza kufikia malengo yake makuu. Kinyume chake, ndio namna kampuni hiyo itakavyojiangusha na kuonekana isiyoendelea na haina mafanikio.

Moja kati ya dhana muhimu katika utamaduni wa kampuni ni kuwa na mfumo wa uamuzi wenye uwazi na ushirikishwaji.

Ushirikishwaji unamfanya mfanyakazi kuhisi kuthaminiwa, kisaikolojia anajiona mwenye kuaminiwa na itasaidia kuongeza ari na ufanisi wa kazi anayopewa. Hekima inahitajika kwa mabosi au wanaongoza kusikiliza maoni ya mfanyakazi wake hata kama yupo katika nafasi inayoonekana ni ya chini kabisa.

Kwa mfano; kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi kuwa na utamaduni wa kujulisha ratiba za vikao, kuhimiza kushiriki, kusikiliza maoni, nini kimeamuliwa, kwa nini imeamuliwa hivyo, na mengineyo. Hii inaweza kutengeneza mazingira mazuri ya mapokeo ya maamuzi na kufanyiwa kazi kwa ufanisi kuliko ikiwa ni “amri kutoka juu”.

Katika dhana nyingine, ni vizuri kwa kampuni kuwa na mtindo wa uongozi wenye kutia ari mtu anapofanya vizuri na kutambua juhudi za ziada za wafanyakazi wake.

Kampuni za biashara mara nyingi huweka matarajio yake wazi na kuainisha majukumu ambayo mfanyakazi anatarajiwa kuyatekeleza. Pia, huwa na utaratibu wa kuchukua hatua za haraka kinidhamu au kurekebisha mambo pale ambapo majukumu hayo hayaendi kama ilivyopangwa, hili si jambo baya.

Hata hivyo, changamoto hutokea pale ambapo mfanyakazi anapotimiza majukumu yake kwa umahiri na hata kuonyesha juhudi za ziada, wakati huo, kampuni haisemi chochote wala kuonesha kuthamini mchango mkubwa mtu aliofanya.

Jambo hili ni kama limeibua dhana mpya katika utamaduni wa uendeshaji taasisi zetu kuwa “ukiona kimya ujue umepatia”. Si sawa, kama mfanyakazi anarekebishwa waziwazi anapokosea, pia aambiwe waziwazi anapopatia “apongezwe”.

Kampuni inaweza kuwa na tafrija za kupongeza wafanyakazi bora kwa wiki, mwezi, mwaka, au tuzo, zawadi, bonasi na mengine. Hayo yatasaidia kuongeza motisha, ari, ubunifu na ufanisi kwa wafanyakazi, bila hivyo kampuni isitafute mchawi”.

Vilevile, ni muhimu kwa kampuni kufanya malipo ya stahiki za wafanyakazi wake kwa wakati, bila kuchelewesha au kuzungusha. Kwa mfano, imezoeleka katika baadhi ya kampuni mishahara kucheleweshwa kwa sababu ambazo hazisemwi, au ikifika wakati wa malipo ya stahiki za kazi mtu aliyofanya ni sharti kulumbana na wahasibu “kuzungusha file”, na si ajabu wakati mwingine kuambiwa “halionekani”, na mengine.

Ikiendelea hivyo, si ajabu wafanyakazi wakawa na morali ndogo. Utamaduni wa namna hiyo unageuka kuwa kama bunduki inayofyatua risasi inayoua kujitolea, ubunifu, na ufanisi kazini. Iwapo hali hiyo itaendelea, kampuni kupata matokeo mazuri na ustawi mkubwa wa biashara inakuwa kama “muujiza”.

Namalizia kwa kusema kwamba wakati kampuni zinapojilinganisha na washindani wao kuhusu matokeo mazuri na kufikia malengo, zinapaswa pia kujiuliza kuwa je, utamaduni wake unachangia ufanisi na utendaji bora? Utamaduni mbovu ni kama zimwi linalofyonza damu ya kampuni taratibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *