Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imelaani pendekezo la awali la Bunge la Israel (Knesset) la kunyakua eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kusema kuwa hatua hiyo inaakisi sura mbaya ya ukoloni wa utawala wa Tel Aviv katika ardhi ya Palestina.

Hamas ilitoa taarifa hiyo jana Jumatano baada ya Knesset kupiga kura ya kuunga mkono muswada ambao utatekeleza sheria ya utawala huo ghasibu katika vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi, pamoja na muswada mwingine unaoidhinisha kunyakuliwa eneo la Maale Adumim. Miswada hiyo lazima ipigiwe kura tatu za ziada katika plenum ili kugeuka kuwa sheria.

Hamas imesema hatua hiyo inaonyesha kuwa Israel inaendeleza juhudi za “kuhalalisha” unyakuzi wa vitongoji vya walowezi na kuweka “mamlaka” yake juu ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, katika ukiukaji mkubwa wa sheria na maazimio ya kimataifa.

Vilevile imeibebesha Israel dhima kamili ya matokeo mabaya ya miswada ya unyakuzi huo, ikitoa wito kwa Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kulaani hatua hizo, kuchukua hatua za kuzuia sera hizo za uvamizi na kuuwajibisha utawala huo kwa jinai zake dhidi ya watu wa Palestina.

“Tunasisitiza kwamba majaribio makubwa ya utawala huo vamizi ya kunyakua ardhi ya Ukingo wa Magharibi ni batili, haramu na kinyume cha sheria,” imesema taarifa ya Hamas na kuongeza: “Hawataweza kubadilisha ukweli kwamba Ukingo wa Magharibi ni ardhi ya Palestina kwa mujibu wa historia, sheria za kimataifa, na maoni ya ushauri yaliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mwaka 2024.”

Mnamo Julai 2024, ICJ ilitoa maoni ya ushauri ikisema kwamba uvamizi wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume cha sheria na lazima ukomeshwe haraka iwezekanavyo.

Katika maoni mengine ya ushauri siku ya Jumatano, mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi, ilisema Israel, kama dola linalokalia ardhi nyingine kwa mabavu, ina wajibu wa kufanya kazi na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwezesha misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, likiwa ni kemeo dhidi ya vikwazo vya kikatili vya utawala huo kwenye eneo hilo la Palestina huku linalokabiliwa na vita vya mauaji ya kimbari. .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *