Madrid, Hispania. Hatimaye, Jude Bellingham ameondoa nuksi ya msimu huu baada ya kufunga bao lake la kwanza kwa Real Madrid katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Juventus katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania.
Kiungo huyo wa England, ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu kuanza kwa msimu, aliipa Madrid uongozi dakika chache tu baada ya kipindi cha pili kuanza akimalizia kwa utulivu pasi kutoka kwa Vinícius Júnior.
Bao hilo lililokuja katika dakika za mwanzo za kipindi cha pili lilikuwa kama ujumbe wa moja kwa moja kwa kocha wa England Thomas Tuchel, ambaye alimwacha Bellingham nje ya kikosi cha taifa mwezi huu licha ya kuwa amerejea kwenye hali nzuri ya kiafya.
Tuchel alidai kuwa alitaka “kudumisha umoja wa kikosi” kilichocheza michezo iliyopita dhidi ya Wales na Latvia, na akasema Bellingham “bado hana kasi ya kutosha.” Kauli hiyo ilizua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa England na wachambuzi wa soka.
“Tunajua Jude ni mchezaji maalum, lakini kwa kambi hii tumeamua kubaki na wachezaji wale wale. Yupo kwenye mpango wetu, ila anahitaji kupata tena kasi yake kamili,” Tuchel alisema mapema mwezi huu.
Bellingham sasa ameonesha jibu sahihi uwanjani si kwa maneno. Uchezaji wake dhidi ya Juventus ulirudisha makali aliyokuwa nayo msimu uliopita, akishirikiana vyema na Vinícius na Kylian Mbappé, waliolitesa lango la Kibibi Kizee hao kutoka Italia mara kwa mara.
Bao hilo pekee lilitosha kuipa Madrid ushindi wao wa tatu mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku Bellingham akionekana kurudi kwenye makali yake baada ya miezi kadhaa migumu.
Hivi karibuni, maisha yake binafsi pia yalitikiswa baada ya kuripotiwa kuwa wazazi wake, Mark na Denise Bellingham, wametengana rasmi baada ya zaidi ya miaka 20 ya ndoa. Ingawa taarifa hizo zilikuwa nzito, Jude hakuruhusu hali hiyo kumvunjia morali akionekana mwenye utulivu na ari mpya kwenye mchezo huo.
Kwa kiwango alichoonesha, ni wazi Bellingham anarejea katika ubora wake wa zamani na sasa macho yote yameelekezwa kwa Tuchel kuona kama atamrejesha kwenye kikosi cha England katika michezo ijayo dhidi ya Serbia na Albania mwezi ujao.