Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa maelekezo ya kisera katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 yanayohusisha utambulisho wa mpigakura.

Maelekezo hayo yametolewa kwa  kuzingatia masharti ya kifungu cha 4, 19(3), 14(2), 84(3)(a) na (b) na 164 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 na kifungu cha 26 cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo yaliyotolewa katika taarifa kwa umami iliyotolewa leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhan Kailima,  mpigakura asiye na picha katika daftari la kudumu la wapiga kura lakini ana kadi ya mpigakura yenye taarifa binafsi zilizomo katika daftari hilo ataruhusiwa kupiga kura.

Mpiga kura ambaye ana kadi yenye namba ya mpiga kura inayotofautiana na namba ya mpiga kura iliyomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini taarifa nyingine zote ikiwemo picha na majina yaliyopo katika daftari hilo  ni sawa kama ilivyo katika kadi ya mpiga aliyonayo ataruhusiwa kupiga kura.

Kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Mpigakura na taarifa zake zipo katika daftari lililopo kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi yake imeharibika, aruhisiwe kupiga kura kwa Kitambulisho cha Taifa (Nida), leseni ya udereva au pasi ya kusafiria.

Hata hivyo, vitambulisho hivyo vitatumika endapo majina yaliyopo katika kitambulisho atakachowasilisha mpiga kura, yatafanana na majina yaliyopo  katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, mpigakura ambaye ana kadi ya kupigia kura lakini taarifa zake hazipo katika daftari la hataruhusiwa kupiga kura.

Aidha kwa wapigakura katika kata 10 zilizofutwa na wapigakura kuhamishiwa kwenye kata nyingine, wataruhusiwa kupiga kura kwenye vituo vipya, licha ya kadi zao kuendelea kusoma taarifa za awali za vituo vilivyofutwa.

Wapigakura hao ni kutoka kata za Kanoge, Litapunga, Katumba, Mtapenda (Kijiji cha Ikolongo na Ndurumo) vilivyopo katika Jimbo la Nsimbo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Kata ya Mishamo, Ilangu, Bulamata na Ipwaga zilizopo katika Jimbo la Tanganyika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Nyingine ni kata za Milambo, Igombemkulu na Kanindo zilizopo katika Jimbo la Ulyankulu Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *