Athens, Ugiriki. Baada ya kusubiri kwa miezi 19 bila kazi ya ukocha, kocha raia wa Hispania Rafa Benítez yuko mbioni kutangazwa rasmi kama kocha mpya wa Panathinaikos ya Ugiriki, ikiwa ni ajira yake ya 17 kama meneja.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65, hajawa na timu tangu alipofutwa kazi na Celta Vigo mnamo Machi 12, 2024, baada ya kushinda michezo mitano pekee kati ya 28 ya LaLiga, na kuacha klabu hiyo ikiwa pointi mbili tu juu ya eneo la kushuka daraja.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ugiriki, Benítez amekubali kandarasi ya miaka miwili na Panathinaikos, klabu ambayo kwa sasa inashika nafasi ya saba kwenye Ligi Kuu ya Ugiriki yenye timu 14, ikiwa na pointi 9 baada ya michezo sita pointi nane nyuma ya vinara PAOK, lakini wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Gazeti la Uholanzi De Telegraaf, linaripoti kuwa mkataba huo utakuwa wa kihistoria nchini Ugiriki, baada ya mazungumzo kufanyika jijini London Jumapili jioni kati ya Benítez na rais wa klabu hiyo Giannis Alafouzos.
Benítez anatarajiwa kulipwa pauni milioni 3.47 (zaidi ya bilioni 7) kwa mwaka, jambo linalomfanya kuwa kocha anayelipwa zaidi katika historia ya soka la Ugiriki.
Hata hivyo, Benítez ameomba muda kabla ya kuanza rasmi majukumu yake ili kukamilisha uhamisho wake kwenda Athens, hivyo hatakuwepo benchi wakati Panathinaikos watakapomenyana na Feyenoord kwenye mechi ya Ligi ya Europa Alhamisi hii.
Kocha wa Feyenoord, Robin van Persie, alionyesha ahueni yake kuhusu hilo akisema:
“Tumefanya maandalizi yetu kwa mujibu wa mbinu za kocha wa muda. Kama Benítez angekuwa tayari amekabidhiwa timu, mambo yangekuwa tofauti kabisa. Kwa upande wangu binafsi, nafuu kwamba bado hajaanza.”
Kabla ya kujiunga na Panathinaikos, Benítez ameziongoza timu mashuhuri duniani kama vile Liverpool, Inter Milan, Chelsea, Napoli, na Real Madrid.
Mafanikio yake makubwa ya ukocha ni pamoja na:
Mataji mawili ya LaLiga na Kombe la UEFA akiwa na Valencia. FA Cup na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Liverpool. FIFA Club World Cup akiwa na Inter Milan pamoja na Europa League akiwa na Chelsea
Orodha ya timu alizowahi kufundisha Benítez:
Real Madrid B (1993–94)
Real Madrid B (1994–95)
Valladolid (1995–96)
Osasuna (1996)
Extremadura (1997–99)
Tenerife (2000–01)
Valencia (2001–04)
Liverpool (2004–10)
Inter Milan (2010)
Chelsea (2012–13)
Napoli (2013–15)
Real Madrid (2015–16)
Newcastle (2016–19)
Dalian Professional (2019–21)
Everton (2021–22)
Celta Vigo (2023–24)
Panathinaikos (2025–)